• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
TAHARIRI: Handisheki bila amani haitoshi

TAHARIRI: Handisheki bila amani haitoshi

KITENGO CHA UHARIRI

MAADHIMISHO ya miaka mitatu tangu Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuweka muafaka wa makubaliano, almaarufu handisheki, yalipita Jumanne bila shughuli nyingi kuihusu.

Viongozi hao wawili walielewana kushirikiana katika mwaka wa 2018 baada ya uchaguzi wa urais ambao ulisababisha mgawanyiko mkubwa nchini.

Katika uchaguzi wa urais 2017, ilikuwa mara ya kwanza Kenya kushuhudia hali ambapo mahakama ilifutilia mbali ushindi wa mgombeaji aliyetangazwa mshindi.

Ilipofika wakati wa kura ya marudio, upande wa upinzani ukiongozwa na Bw Odinga chini ya Muungano wa National Super Alliance (NASA) ulikataa kushiriki uchaguzini.

Matukio hayo yote, pamoja na uamuzi wa Bw Odinga kujiapisha kama ‘rais wa wananchi’ baadaye yaliweka taifa hatarini kutumbukia katika ghasia.

Ni kwa ajili hii ambapo wananchi wengi na washirika wa kimaendeleo katika taifa hili walisifu uamuzi wa viongozi hao wawili.

Wengi walihofia kuwa bila ushirikiano, nchi ingezama katika fujo na vita sawa na au mbaya kuliko zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa 2017.

Athari ya fujo hizo huwa ni maafa, hasara inayotokana na uharibifu wa mali, na kuzorota kwa uchumi kwa vile wawekezaji huogopa nchi zilizojaa fujo.

Ijapokuwa kuna wapinzani wa handisheki ambao walijitwika jukumu la kuwa viongozi wa upinzani dhidi ya serikali, si siri kuwa hali imekuwa tulivu kisiasa ikilinganishwa na kama hapangekuwepo mwafaka huo wa Rais na Bw Odinga.

Hata hivyo, sasa inaonekana mambo yameanza kurudi kinyume kwani wanachama wa ODM wameibua lalama kuhusu uhuru na haki katika uchaguzi. Lalama hizo zinaibua ishara kwamba, ingawa nchi imekuwa tulivu kiasi cha haja kufikia sasa, tungali tunakodolea macho machafuko yanayohusiana na uchaguzi tunapoelekea mwaka wa 2022.

Tunatoa wito kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wadhihirishie wakosoaji wao kwamba ushirikiano wao ulilenga kuwa wa manufaa kwa taifa zima, kwa kuhakikisha kutakuwa na mfumo utakaowezesha uchaguzi kusimamiwa kwa njia ya haki katika miaka ijayo.

Itakuwa ni aibu kama rasilimali zote zilizotumiwa kufanikisha handisheki zitapotea bila mafanikio yoyote kupatikana.

You can share this post!

JAMVI: Kipute kikali kati ya Rais Kenyatta na Ruto...

WASONGA: Serikali itenge fedha kununua dozi zaidi za chanjo...