• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
KINA CHA FIKRA: Kujiamini kama kiambata cha ufanisi maishani

KINA CHA FIKRA: Kujiamini kama kiambata cha ufanisi maishani

Na WALLAH BIN WALLAH

WATU wengi wana uwezo wa kuyatenda mambo mazuri makubwa maishani lakini wanashindwa kwa sababu hawajiamini!

Wanadhania ati wangekuwa kama akina fulani fulani ndipo wangeyatenda matendo mazuri makubwa yenye sifa na faida mzomzo ulimwenguni!

Leo nikwambie hivi: Wewe ni wewe! Usiogope kuwa wewe! Mwenyezi Mungu alikuumba hivyo ulivyo kwa uwezo wake akakupa akili, ubora na umuhimu wako maishani!

Ukijiamini utajifanyia mambo yako yote na shughuli zako zote vizuri zaidi mpaka ufanikiwe bila ya kungojea uwe fulani au uwe kama fulani! Wewe ni wewe! Amua unachotaka na unavyotaka kuwa kwa kujiamini kwamba una uwezo! Kujiamini ndiko kutekeleza wajibu!

Mtu anapojiamini huongeza ujasiri moyoni na busara kichwani. Mfano mzuri ni wa kijana mdogo Daudi mwana wa Yesse ambaye alimshinda Goliati kwa sababu ya kujiamini na kuamini kwamba alikuwa na uwezo wa kumpiga Goliati na kumwangusha chini licha ya ukubwa wake, unene wake na urefu wake! Daudi aliamini kwamba katika mapambano usijione kwamba u mdogo! Usijidunishe na kusema ati lazima uwe jitu kubwa ndipo ushindane upate ushindi!

Katika mapambano binadamu anahitaji imani na uwezo wa akili za kupambana wala si ukubwa wa mwili na kifua kipana cha kupambana. Ukijiamini kwamba unaweza lazima utaweza! Katika imani na kujiamini kwako pia uongezee nia ya matendo ili utende kwa vitendo! Lakini kujiamini kunampa mtu msukumo, ari, ghera, motisha, kichocheo na hamasa za kutaka kuendelea kutekeleza wajibu hadi ufanikiwe! Usiwe na unyonge wa kukata tamaa! Usikubali kushindwa kabla ya kujitahidi kujaribu! Jiamini!!

Mtu anayefanya kazi kwa kujiamini siku zote kazi zake huwa njema na zenye mafanikio mazuri zaidi! Mti mwema ndio uzaao matunda mema!

Vivyo hivyo, mwanafunzi anayesoma kwa kujiamini kwa nia moja, hupata mafanikio na matokeo bora zaidi! Na siyo matokeo pekee katika mtihani, bali kuelewa kwake huwa imara na kwa kiwango cha juu sana! Kwa mfano sasa hivi tumo katika msimu wa mtihani.

Wewe mwanafunzi unapaswa kuwa na imani na kujiamini kwamba umekuwa shuleni muda wote huo ukisoma, walimu wapo, vitabu vipo, afya unayo na akili unazo kichwani! Kwa hivyo mtihani utakapoletwa, uyasome maswali uyaelewe kisha ujibu kila swali kulingana na jinsi ulivyoulizwa! Toa jibu linalotakikana linalowiana na swali! Usijibu unavyofikiria wewe! Ujiamini!

Ndugu wapenzi, leo namalizia kina cha fikra kwa kunukuu kwamba, “Katika mashindano ya mbio za masafa marefu dhidi ya Kobe na Sungura, Kobe alimshinda Sungura kwa kujiamini tu wala siyo kwamba alikuwa na mbio sana!” Amua! Ukijiamini utapata ushindi na mafanikio bora maishani! Jiamini!!!!

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Beatrice Gatonye

NASAHA: Nukta muhimu za kuzingatia mitihani ya kitaifa...