• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
NDIVYO SIVYO: Matumizi uchwara ya kiunganishi ‘kama vile’

NDIVYO SIVYO: Matumizi uchwara ya kiunganishi ‘kama vile’

Na ENOCK NYARIKI

“KATIKA uwanja wa ndege wa Nyerere, wafanyakazi hawakuwa wamevaa barakoa na waliendelea na maisha kama vile hakuna korona.’’

Sentensi hii inajitokeza katika taarifa inayohusu kupuuzwa kwa kanuni za afya na jinsi mapuuza yenyewe yalivyochangia kuenea kwa maradhi ya korona nchini Tanzania. Ingawa kisarufi, maneno ‘endelea na maisha’ hayana mantiki, yanapotumiwa katika mawasiliano ya barabarani, huenda yakafanikiwa kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa. Lipo kosa jingine la sarufi linalojitokeza katika sentensi tuliyoinukuu na ambalo litakuwa kitovu cha mjadala wetu. Kiunganishi ‘kama vile’ hakifanikiwi katika kuziunganisha kauli ‘wanaendelea na maisha’ na ‘hakuna korona’.

‘Kama vile’ ni kiunganishi ambacho kimeundwa kwa maneno mawili ambayo ni ‘kama’ na ‘vile’. Neno kama ni la kategoria mbili: kiunganishi na kitenzi. Kama kiunganishi, huibua maana tano ila maana moja tu ndiyo itakayotufaaa katika maelezo yetu. Hutumiwa kulinganisha vitu viwili. Tutaifafanua hoja hii baadaye katika makala haya ila kwanza tueleze maana za neno ‘vile’. Vile ni kivumishi cha kuashiria katika ngeli ya KI-VI ambacho huonyesha vitu vilivyo mbali na mzungumzaji. Neno hili pia hutumiwa kama kielezi cha namna mfanano kuelezea namna ya kutendekea kwa kitendo au vitendo fulani. Mfano: Wezi walituvamia vile wakati wa usiku.

Kuna tofauti finyu sana baina ya kiunganishi ‘kama vile’ na ‘kwa mfano’. Viunganishi vyote viwili hutumiwa wakati wa kutaja au kuorodhesha vitu vichache kati ya vingi vinavyozungumziwa. Kiunganishi ‘kana kwamba’ nacho hutumiwa kulinganisha mambo mawili ambapo jambo la pili hutendwa kwa kulipuuza, kutolizingatia au kutolitilia manani lile la kwanza ambalo ndilo muhimu zaidi. Aghalabu, kiunganishi hiki hutumiwa kwa njia hasi katika ulinganishaji wa aina hiyo. Mfano: Kwa nini unamtesa mtoto huyo kana kwamba hana wazazi? Katika mfano huu, mambo mawili yanajitokeza. Kwanza, anayeteswa ana wazazi. Pili, kitendo (kutesa) kinatendeka kwa kupuuza jambo la kwanza ambalo ni ukweli kwamba anayeteswa ana wazazi.

Sentensi tuliyoitanguliza katika makala haya ilipaswa kuandikwa hivi: “Katika uwanja wa ndege wa Nyerere, wafanyakazi hawakuwa wamevaa barakoa . Waliendelea na shughuli zao za kawaida kana kwamba hakuna ugonjwa korona.’’

Alhasili, ijapokuwa ‘kama vile’ hutumiwa katika mazungumzo kulinganisha mambo mawili ambapo jambo la pili hutendeka kwa kulipuuza, kutolizingatia au kutolitilia maanani lile la kwanza ambalo(la kwanza) ndilo muhimu zaidi, kiunganishi kinachopaswa kutumiwa katika mazingira hayo ni kana kwamba.

You can share this post!

Afisa wa GSU aangamiza wenzake wawili kwa risasi na...

VITUKO: Munira na walimu wachache wapanga kuwapunja wenzao...