• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
VITUKO: Munira na walimu wachache wapanga kuwapunja wenzao pesa za kampeni

VITUKO: Munira na walimu wachache wapanga kuwapunja wenzao pesa za kampeni

Na SAMUEL SHIUNDU

MUNIRA alijitia hamnazo tangu kupokezwa pesa na wawaniaji mbalimbali wa chama cha kutetea walimu.

Kimya hiki kiliwababaisha walimu wenzake ambao waliamini kuwa kimya kikuu hujiri kabla ya mshindo. Hawakujua ni mshindo wa aina gani huo ambao ungewapata baada ya kunyamaziwa na huyo mweka hazina wao. Hawakujua alilokuwa akiwapangia. Laiti angewaambia jambo, labda roho zao zingetulia. Lakini aliufyata tu.

Kadri siku zilivyoyoyoma na siku ya upigaji kura kukaribia, ndivyo kimya cha mweka hazina huyo kiliendelea kutawala. Walimu wengine walianza kuulizana alikoutoa huu ujasiri wa kuwanyamazia. “Yawezekana kwamba dada Munira kasahau kuhusu hizi pesa zetu?” Pengo alimuuliza mwenzake siku moja. “Ukweli ni kwamba tunapangiwa mafamba. Wewe huoni kila mtu katulia hata wale ambao wanajulikana kwa kuwa bingwa wa kudai haki zao. Labda washamegewa tonge lao. Ukiona vyaelea jua kuwa vimeundwa kaka.”

Huku baadhi ya walimu wakijiuliza kuhusu hatma ya pesa za kampeni, mwalimu Munira na rafiki zake walikutana kujadili jinsi ya kugawana hela hizo kwa njia ambayo ingewaacha na kibaba kizuri

Shule ya Sidindi ilikuwa na walimu takriban hamsini, ukiongeza waliokuwa kwenye majaribio ya ufundishaji utapata jumla ya walimu sitini. Sitini hawa wakigawiwa elfu kumi na mbili zilizotolewa na wawaniaji, ilikadiriwa kuwa kila mmoja wao angepata shilingi mia mbili tu. Pesa hizi zilionekana chache mno kwa Munira na wenzake. Ilibidi njama ipangwe.

Mmoja wa walimu akapendekeza kuwa pesa hizo zipewe walimu walioajiriwa na tume pekee yao, lakini nao pia hawakuwa wachache. Mwingine akazua pendekezo tofauti, zipewe tu walimu wanachama wa chama hicho cha kutetea maslahi ya walimu. Hawa nao hawakuwa wachache jinsi ilivyodhaniwa. Ilibidi njama zaidi ya kibaguzi ipangwe. Ndipo Munira alivyozua pendekezo.

Munira alipendekezea wenzake kuwa pesa hizo zipewe tu wale wanachama ambao wangeenda kupiga kura. “Si vyema tupokee pesa na tukose kushiriki zoezi la kura. Huko ni kujipaka tope. Pesa hizi zafaa kupewa walimu watakaoenda kupiga kura ili wazitumie kama nauli ya kuwarejesha makwao” Dalili ya mvua ni mawingu.

Pengo alishuku njama. Alijua kuwa pesa hizi zilikuwa za kampeni na wala si za nauli. Alijua kuwa Munira alilenga kuwatenga wengi ambao hawangeenda kupiga kura. Pengo alijua njama hii ilinuiwa kuwabagua baadhi yao lakini akaufyata tu.

Hakutaka kuonekana kama wana wa giza wanaozozania mambo ya dunia.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Matumizi uchwara ya kiunganishi ‘kama...

Obiri, Brigid wala sifa kedekede Siku ya Wanawake Duniani