Jombi ‘afilisisha’ shugamami

Na JOHN MUTUKU

LAVINGTON, NAIROBI

SHUGAMAMI mtaani hapa alitiririkwa na machozi ya majuto baada ya barubaru aliyemteka kimapenzi, kumcheza shere na kutoweka na mamilioni ya pesa na mali yake.

“Jamani mbona sina kismati maishani? Nitaitoa wapi mali na pesa zangu alizoondoka nazo?” Shugamami alilia huku akizongwa na mawazo.

Inasemekana mama alikutana na jamaa huyo katika hafla moja jijini. Polo ambaye alikuwa MC wa sherehe alimvutia shugamami huyo kwa sauti yake nyororo. Alikuwa pia na sura nzuri pamoja na maumbile ya mwanamume mnyanyua vyuma.

Baada ya kubadilishana nambari za simu, walianza kuwasiliana na penzi likanoga kweli. Na ili kumthibitishia ukweli wa mahaba, shugamami huyo alimnunulia polo nyumba ya kifahari, gari aina ya BMW pamoja na kuikuza akaunti yake kwa mamilioni kadhaa.

“Kipenzi, wewe ndiwe wangu ila nina wivu sana. Sitaki kukuona na mwengine ndio maana nimewekeza kwako kwa mali nyingi. Huba ni kuaminiana,” shugamami alisema.

“Haina tabu. Nimetambua wanipenda nami naapa kulitunza, kulipalilia na kulilinda penzi letu daima,” polo alimhakikishia.

Haukupita muda mrefu, polo aliingiwa na tamaa. Alianza kuandamwa na mademu wengi kutokana na pesa alizokuwa nazo.

“Mbona unazidi kujifunga kwa ng’ombe yule. Mama wa miaka hamsini na moja mtapelekana wapi? Tuondoke nje ya nchi tukaponde maisha,” totoshoo mmoja alimshauri.

Hapo ndipo akili ya polo ilipozinduka akauona mpango huo ukiwa bora. Aliiuza nyumba kisiri pamoja na mali nyingine kisha alfajiri moja akatoweka na kuzima simu.

Shugamami alijaribu kwa siku nyingi kumpigia asimpate. Hivyo ndivyo polo alivyotoweka na kumwacha shugamami mataani.