• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
TAHARIRI: Kafyu: Mwelekeo wahitaji busara

TAHARIRI: Kafyu: Mwelekeo wahitaji busara

KITENGO CHA UHARIRI

NI takriban mwaka mmoja sasa tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kugunduliwa humu nchini.

Gonjwa hili ambalo kitovu chake ni mjini Wuhan, China liliumiza biashara na chumi za ulimwengu mzima na kusababisha vifo ambavyo havijawahi kutokea katika historia ya nchi mbalimbali duniani.

Kulikuwa na kila sababu ya Wakenya, na walimwengu wote, kuwa na wasiwasi kutokana na athari za janga hilo.

Karibu mwaka mmoja baadaye, Wakenya wanafanya kila wawezalo kuibuka kutoka kwenye majivu ya kipindi kibaya zaidi katika historia ya nchi. Watu wengi walipoteza kazi, wengi walifariki na matatizo chungu nzima.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutoa mwelekeo wa nchi kuhusu kafyu aliyoiweka tangu mwanzoni mwa Januari. Kafyu hiyo imedumu kwa miezi mitatu na sasa ni jukumu lake kutoa mwelekeo mwafaka ili kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele.

Wakati huo huo, kamati ya Kitaifa kuhusu Kukabiliana na Virusi vya Corona pamoja na Kamati ya Kutoa Ushauri kuhusu Usalama wa Kitaifa (NSAC) zinatarajiwa kumshauri Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa kafyu atakapohutubia taifa kesho.

Kamati hii inahisi kwamba pana haja ya Rais kuendeleza kafyu ili kukabiliana na wimbi jipya la corona ambalo linasemekana kuwa hatari zaidi.

Akishauriwa hivyo, ni wazi kuwa hatua atakayochukua itaendelea kutatiza biashara kadhaa hasa za starehe.

Baa, mikahawa, mahoteli na hafla mbalimbali zitazidi kutatizwa kutokana na hatua hiyo. Kamati hizo zinahoji kuwa idadi ya maambukizi imeanza kupanda.

Pia wanasema kuwa mataifa mengine duniani bado hayajafunguliwa tena. Tathmini ya mifumo ya afya nchini imeonyesha kuwa hospitali nyingi zimeanza kupata idadi kubwa ya wagonjwa wanaotafuta matibabu ya Covid-19. Uhuru anapaswa kutumia busara yake anapofanya maamuzi kuhusu kafyu, asiumize biashara na pia azingatie wimbi jipya la Covid-19.

Tunaweza tu kutumai kwamba kutokana na hali ya awali ambayo imefanya idadi kubwa ya wananchi kuwa na kinga, upeo na kiwango cha kusambaa hakitakuwa kibaya zaidi kushinda wimbi la pili ambapo tulikuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo na wagonjwa waliolazwa hospitalini.

You can share this post!

Wasiwasi wakulima wa mahindi kugeukia miwa

KAMAU: Kenya ihakikishe amani yake itaendelea kudumu