• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
KAMAU: Kenya ihakikishe amani yake itaendelea kudumu

KAMAU: Kenya ihakikishe amani yake itaendelea kudumu

Na WANDERI KAMAU

MATUMAINI ya kila mtu anapoanza safari ni kufika anakoelekea akiwa salama. Tumaini jingine huwa ni kutimiza malengo anayokusudia anapoanza safari husika.

Taswira hiyo ndiyo iliyokuwepo nchi nyingi za Afrika zilipopata uhuru wao katika miaka ya sitini.

Matumaini yazo yalikuwa kufikia kilele cha kiuchumi, kisiasa na kijamii baada ya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Hakuna nchi hata moja iliyokusudia kukumbwa na mikasa kama kuchipuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwenye ‘safari’ ya kufikia malengo yake.

Hata hivyo, safari za mataifa mengi zilivurugika. Zilikumbwa na ‘ajali’ njiani. Ajali zilizoanza kama mkasa mdogo ziligeuka kuwa majanga makubwa na mawimbi yaliyoyasomba mataifa hayo kwenye bahari za uadui, majeraha, mapinduzi ya kijeshi na maafa.

Baadhi ya nchi zilizojipata kwenye mikasa hiyo ni Somalia, DRC Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Uganda, Nigeria kati ya zingine.

Somalia iliangukiwa na mkosi wake mnamo 1991, baada ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Mohamed Siad Barre kung’atuliwa mamlakani kwenye mapinduzi ya kijeshi.

Mapinduzi hayo yaliendeshwa na koo kadhaa ambazo hazikuwa zikiridhishwa na ungozi wake. Tangu wakati huo, Somalia iligeuka kuwa kama Jehanamu ya Kidunia. Haijawahi kupata amani hata kidogo.

Juhudi za kurejesha amani na uthabiti wa kisiasa nchini humo hazijakuwa zikifaulu kutokana na chuki, ushindani wa kisiasa na kimamlaka miongoni mwa koo husika.

Nchini DR Congo, misukosuko ilianza mara tu baada ya mauaji ya waziri mkuu wake wa kwanza, Patrice Lumumba, mnamo Januari 17, 1971. Ilidaiwa mauaji hayo yaliendeshwa na washindani wake kisiasa, kwa usaidizi wa mataifa ya kigeni. Baadhi ya vitabu vya historia vimekuwa vikiitaja Ubelgiji kuwa mhusika mkuu wa mauji hayo.

Kama Somalia, taifa hilo limekuwa likikumbwa na mizozo ya kisiasa isiyoisha hadi leo.

Simulizi kama hizo ndizo zinayaandama mataifa mengi yanayokabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kikabila.

Licha ya mielekeo hiyo kushuhudiwa katika nchi zingine barani humu, Kenya haijasazwa hata kidogo. Imekuwa ikiathiriwa na ghasia za kikabila ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1992.

Licha ya kukumbwa na mikasa kama hiyo awali, tunaonekana kutojifunza lolote.

Dhihirisho la haya ni ghasia zilizoshuhudiwa kwenye chaguzi ndogo zilizokamilika wiki iliyopita katika maeneobunge ya Matungu (Kakamega) na Kabuchai (Bungoma).

Inasikitisha kuwa matukio hayo yalitokea wakati tunajitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kwa utathmini wa kina, mwelekeo kama huo ulishuhudiwa mwaka 2005, baada ya kura ya maamuzi yenye ushindani mkubwa kati ya kambi za ‘Ndio’ na ‘La.’

Baada ya matokeo ya zoezi hilo kutangazwa na Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK), serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki ilishindwa vibaya na upinzani, ulioongozwa na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Taharuki ya kisiasa iliyotokea ndiyo ilijenga ghasia za mwaka 2007/2008, ambapo zaidi ya Wakenya 1,300 walipoteza maisha yao.

Tusikubali mikosi ya nchi zingine kutuandama. Tumalize ‘safari’ yetu kwa njia salama.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Kafyu: Mwelekeo wahitaji busara

AKILIMALI: Aliacha ubawabu sasa anapepea katika kilimo cha...