FAIDA YA UBUNIFU: Hajuti kuacha kazi ya benki na kujiajiri na pia kufunza wengine kazi ya mkono

Na HAWA ALI

INGAWA hakuwa na elimu ya namna ya kutengeneza viatu na soko lake, Vitalis Omondi, aliyekuwa mfanyakazi wa benki, aliamua kubadili mwelekeo kwa kuanzisha kampuni ya viatu iitwayo Odhis Shoes.

Aliianzisha kampuni hii eneo la Kibra, Nairobi mwaka 2015, kisha mwaka mmoja baadaye alijiuzulu kazi yake ya ukarani katika benki ili aiendeleze. Baadaye aliajiri wafanyakazi wanne wa kudumu, akiwemo mtaalamu mmoja wa kutengeza viatu aliyejifunza kutoka kwake na pia kuwafunza wengine.

Aliianzisha kampuni hiyo ya viatu kwa mtaji wa Sh100,000 (alizokuwa akiweka akiba), kununua ngozi na malighafi mengine, kulipia mahali pa kazi.

Vitalis anakiri kuwa ingawa biashara ya kuuza viazi ina ushindani mkubwa, anasisitiza kuwa, “Ushindani ni mzuri wakati wote ila si rahisi kumudu, hivyo ninahakikisha kampuni yangu mara zote inatengeneza bidhaa nzuri ili ziweze kupendwa kwa namna tunavyotaka.”

Anasema kuwa wateja wengi hupendelea kununua nembo maarufu ya viatu na vingi hutoka China lakini haonekani kutishiwa nazo.

“Nimejiwekea kanuni mimi na ninaofanya nao kazi, kanuni ambazo zinanisaidia kupenya katika soko la viatu kwa urahisi,” akadokeza.

Kuwafanya wateja kuwa marafiki ni jambo analotilia mkazo Vitalis. Wateja wake wengi ni wakazi wa Nairobi lakini pia wengine hutoka maeneo mbalimbali kama Thika, Naivasha, Nakuru na wengine pia hutumiwa viatu.

“Nina wateja wengi ambao wengi huja hapa dukani kununua lakini wengine hutumiwa kama mzigo kwa basi,” aliongeza. Anasema kuwa sasa hivi anaandaa tovuti ya E-Commerce kuweza kumsaidia kuuza viatu vyake kwa njia ya mtandaoni.

Pia, yeye hununua viatu vingine zaidi ya vile anavyotengeneza na kuuzia baadhi ya wateja wake.

Vitalis anadokezea Akilimali pia kuwa ana kundi lingine la wanunuzi ambao hununua viatu vyake kwa bei ya chini kidogo na kwenda kuuza kwa bei rahisi.

Bei ya viatu hulingana na muundo, na aina ya ngozi iliyotumiwa pale, lakini yeye huuza kati ya Sh800 hadi 4,000.

“Ninauza pia viatu vya shuleni ambavyo huuzika sana wakati shule zinafunguliwa. Janga la corona lilituathiri sana kwa sababu shule zilikuwa zimefungwa, hivyo hatukuuza sana,” asema.

Mafundi wake wa viatu wamekuwa wakitoa mafunzo kwa watu wanaotaka kujifunza kuhusu utengenezaji wa viatu na kazi nyingine za ngozi, na kuwafundisha namna ya kupata wateja kwa mitindo ya aina mbalimbali ya bidhaa lakini kwa ada fulani, si bure. Kwa ufupi ni kuwa karakana yake Omondi pia ina kitengo cha kutoa mafunzo kwa wanaotaka kujifunza kuhusu uundaji viatu.

Alipata wanafunzi wengi katika kipindi cha corona na hivi sasa hachukui wengine tena hadi mwaka 2022.

Changamoto kwake ni nafasi ya kutolea mafunzo hayo, lakini anaahidi kutafuta jumba kubwa zaidi la kuendeshea shughuli hiyo.

Vitalis anasema kwa bashasha kuwa hajutii kuacha kazi ya benki kwa sababu mshahara alioupata ulikuwa mdogo zaidi ikilinganishwa na kibaba akipatacho sasa hivi. “Nilikuwa ninapata Sh30,000 kwa

mwezi, pesa ambazo hazingenikidhia mahitaji yangu, lakini kwa sasa, hela ninazopata si mbaya, na pia ninaweza kulipa wafanyakazi wangu wote kwa wakati mzuri bila shida yoyote,”alisema.