• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
KINYUA BIN KING’ORI: Vijana waombe msaada kwa jamii badala ya kujitoa uhai

KINYUA BIN KING’ORI: Vijana waombe msaada kwa jamii badala ya kujitoa uhai

Na KINYUA BIN KING’ORI

INASIKITISHA na kuhuzunisha sana kuona vijana wetu wakijiua kwa kujitia vitanzi au kunywa sumu.

Visa hivi vimekithiri katika kijiji cha Ntobuine, eneobunge la Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru. Ingawa visa kama hivi vinaripotiwa kutoka pembe zote za nchi, nahisi kuwa katika jamii yetu vimezidi na sasa vinatishia hata maendeleo ya kijamii.

Nimeshindwa kuelewa kwa nini kijana anayeweza kujitegemea katika maisha yake bila usumbufu au kutegemewa katika juhudi za kufanikisha mambo muhimu katika jamii anaweza kuchukua hatua ya kujiua.

Kuna zaidi ya vijana wanne ambao wamejiua katika kipindi cha miezi saba na vifo.

Jamii ikiongozwa na wazee wakishirikiana na viongozi wa kisiasa na serikali wanapaswa kuchukua hatua ya dharura kuzungumzia tabia hiyo ili kuzuia vifo zaidi. Tumechoka kuomboleza vifo vinavyoweza kuzuiwa.

Imebainika kuwa wengi hujitia kitanzi wanaponyimwa urithi mapema hasa wa mashamba ya miraa, baada ya kulemewa na changamoto za maisha.

Ni wajibu wa jamii hasa kina baba kujitokeza kushauriana na watoto wao wa kiume kuwa wanaweza kujitegemea na kufaulu maishani bila kupata urithi wa shamba la miraa au kupitia msaada wa mzazi.

Japo sipingi wazazi kugawa ardhi na mali kwa wana wao, tunaweza kubadili mwelekeo huo kwa kushauri watoto kuhusu njia mbadala za kujitegemea.

Vijana wanafaa kuelezwa kuwa changamoto za maisha ni kawaida na wanachopaswa kufanya kwa wenye uvumilivu.

Hata hivyo, kinachokera zaidi ni kuona jamii imenyamaza kama kwamba vifo hivyo si pigo kwetu.

Jamii inataka watu waendelee kujiua hadi wafikie wangapi ili wazinduke na kuchukua hatua? Ikiwa tutakaa na kukosa kujadliliana mapema juu ya swala hilo, nahofia tutawapoteza vijana wengi.

Kila mzazi ana jukumu la kuwajibikia usalama wa mtoto wake kwa kushughulikia mahitaji yake na na anapoingia utu uzima, kuna mila na tamaduni zinazofuatwa kumrithisha ali ili aweze kujisimamia.

Wazazi wanafaa kujua jinsi ya kuongea na wana wao hasa wanapodai urithi au msaada kutoka kwao badala ya kuwakaripia.

Naomba kama jamii turudie mila na desturi zetu ambapo kulikuwa hata nba vikao vya kujaili mambo yanayoimkumba jamii, ni ni kimaadili, kiuchumi miongoni mwa mengine.

Tunafaa kuelewa maarifa ambayo wazee walitumia kushughulikia changamoto mbalimbali katika jamii. Ni muhimu hata hivyo kwa kila mmoja kuchangia juhudi hizi na kuzuia vijana wetu kujiangamiza.

You can share this post!

BIASHARA MASHINANI: Mwalimu aliyeona nafasi ya ujasiriamali...

Diwani ageuka mpishi wa kuchuuza chakula