Kisura avua kalameni kila kitu!

Na JOHN MUTUKU

ROYSAMBU, Nairobi

POLO wa hapa amebaki hohehahe baada ya kuibiwa mali yote ya nyumba na mpenzi waliyefahamiana mitandaoni.

Jamaa ni kapera, hivyo marafiki walimshauri kutafuta mchumba kwenye mitandao baada yao kujaribu na mambo kuwaendea vyema.

“Mambo ya zamani ndugu yashapitwa na wakati. Jitose mitandaoni utafute kichuna wa kukupikia, kukufulia nguo na kukutoa baridi,” mmoja wa rafiki zake akashauri.

Baada ya muda, polo alimpata totoshoo aliyemvutia kwenye mtandao mmoja.

Siku moja demu akamwarifu kuwa angependa kumtembelea.

Kaka alijiandaa kwa kunadhifisha nyumba na jioni hiyo mgeni akaingia.

Jamaa alipomuona, alishtuka lakini akajituliza. Inasemekana mwanadada aliyefika kwake alikuwa tofauti na picha iliyokuwa mtandaoni.

Mgeni alikuwa jimama la takriban miaka arubaini hivi, nene lenye mwili tipwatipwa.

Hakuwa msichana wa rika lake bali shugamami wasioweza hata kutembea barabarani pamoja.

Polo alijikaza kupika na walipokula na kuzungumza zaidi, akatoa masharti.

Alitaka mgeni alale kitandani naye kwenye kochi. Mgeni hakustaajabu hata!

Usiku huo, polo hakupata lepe la usingizi.

Siku iliyofuata alienda kazini akidhamiria kunyoosha mambo baina yao usiku huo akipanga kumfukuza mwanamke huyo.

Ajabu ni kuwa aliporejea jioni, hakumpata au chochote cha thamani katika nyumba yake.

Si redio, si runinga, si sofa si vyote; vyote havikuwemo.

Jamaa aligutuka kwamba alikuwa ameangukia jambazi akisaka mpenzi mtandaoni.

“Wajinga ndio waliwao. Huu ni msiba wa kujitakia. Unawezaje kumwalika mgeni kwako na kuondoka uende kazini ukimwachia nyumba yenye vyombo ghali?” sauti ilimkumbusha.

Inadaiwa siku hizi kalameni ameanza maisha upya, akijutia uamuzi wa kusaka mrembo kupitia mitandao.