• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Covid-19: Hisia za baadhi ya Wakenya kuhusu kafyu

Covid-19: Hisia za baadhi ya Wakenya kuhusu kafyu

Na WANGU KANURI

JANGA la Covid-19 liliingia bila kubisha hodi nchini Kenya mnamo Machi 2020 na kuvuruga pakubwa vitega uchumi vya watu huku kampuni nyingi zikiwapiga kalamu wafanyakazi wao.

Isitoshe, walioponea kutofutwa mishahara yao ilipunguzwa. Shule zote nchini zilifungwa huku ikiwalazimu wakuu wa taasisi hizi kuwa na njia mbadala za kukidhi kiu cha masomo kwa wanafunzi. Biashara zinazomilikiwa na watu binafsi na hali kadhalika, zilipata pigo kwani baada ya uchumi kudorora, watu walilazimika kubadilisha vitengo mbalimbali vya matumizi yao huku wakivipa vitengo vyenye umuhimu sana kipaumbele.

Ili kudhibiti mkurupuko wa ugonjwa huu, serikali kupitia wizara ya afya iliweka mikakati kadha wa kadha. Kwanza, wananchi walilazimika kuvaa maski ama ukipenda barakoa kila wakati wakitangamana na wenzao. Pili, watu walipaswa kuhakikisha kuna urefu wa mita moja na nusu baina yao na mwenzao. Tatu, watu walihitajika kunawa mikono au kutumia viyeyushi. Nne njia ya kusalimiana ilibadilika kwani hatukuruhusiwa kugusana. Mwisho kama njia ya kudhibiti kutangamana kwa watu, kafyu iliwekwa.

Japo kanuni hizi zilisaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wa virusi hivi; hali ya maisha ya watu itachukua muda kabla kurejea kama ilivyokuwa hapo awali.

Tujapongojea kwa hamu na ghamu tamko la Rais kuhusu kuondolewa ama kutoondolewa kwa kafyu Ijumaa, haya ni baadhi ya maoni kutoka kwa watu wanaowakilisha nyanja kadha wa kadha na maoni yao kuhusiana na jinsi maisha yao yalivyobadilika aidha kichanya au hasi baada ya janga la Covid-19 kufanya makao yake nchini Kenya.

Ninawasiliana naye Ann Mburuga, mwalimu wa fizikia na hisabati katika shule ya sekondari. Kwake kama mwalimu, ugonjwa huu wa corona ulimfaa sana kwani alipata nafasi ya kupata mapumziko bora.

Akieleza Taifa Leo Bi Mburuga anasema, “Tangu niajiriwe kama mwalimu yasibu zaidi ya miaka 20 iliyopita, imekuwa vigumu sana kupata muda wa mapumziko zaidi ya zile nyakati ambazo shule hufungwa. Hii ni kwa sababu nyakati za likizo mtu hujishughulisha na mengi na akakosa kujitengea wakati bomba wa kupumzika. Baada ya corona kufika nchini na kanuni za nchi kuhusiana na kudhibiti uenezi wa virusi hivi kuwekwa, niliweza kupumzika ifaavyo.”

“Isitoshe, licha ya serikali kuendelea kutulipa mishahara yetu, ushuru ulipunguzwa hivi basi mshahara ukawa mwingi kidogo. Hata hivyo, majukumu yetu yaliongezeka haswa pale ambapo kazi au biashara za wenzi wetu ziliathirika. Vile vile, niliweza kuyakidhi mahitaji ya wanafamilia wangu kwa kuwapa muda wa kutangamana nao jambo ambalo lilikuwa ngumu kufanya hapo awali. Kwangu naipongeza serikali kwa kuhakikisha kuwa hatujathirika sana,” akasema.

*David Maina* ambaye hili si jina lake rasmi, ni muuguzi katika hospitali mojawapo nchini Kenya.

Ugonjwa huu wa Covid-19 ulipothibitishwa mara ya kwanza kuwa nchini, mimi kama muuguzi nilifadhaika sana. Hii ni kwa sababu, mosi huu ni ugonjwa ambao kamwe hujawahi onekana ama kuwa duniani na pili picha ambazo zilikuwa zinaenea katika mitandao ya kijamii kutoka nchi ambazo ugonjwa huu ulifika kwanza. Mambo haya mawili yalituadhiri sana sisi kama wauguzi huku mtu akishangaa la kufanya.

“Mimi kilichonipa msukumo wa kuenda kazini ni kule tu kupenda kazi yangu. Siwezi nikasema kuwa mshahara hata ulinishawishi kwani hata kabla ya janga la corona, maandamano yamekuwa njia yetu ya kuzipigania haki zetu. Isitoshe, hata baada ya kaunti kufungwa ugumu wa kufika kazini ulikuwepo hata ingawa niliruhusiwa kuvunja kanuni za kafyu,” alieleza.

“Ugonjwa huu ulinitia kiwewe haswa kabla ya hadithi za uongo na dhana potovu kuhusiana na ugonjwa huu kuchambuliwa ki mchele na ndume. Baada ya idara ya afya ulimwenguni (WHO) kueleza yaliyokweli kuhusiana na ugonjwa huu, sisi kama wauguzi tuliweza kupunga hewa. Kwetu haikutushtua sana, tuliichukulia kama homa hivi basi mtu anaweza kupona iwapo atazingatia maoni ya daktari. Hali kadhalika, nilipoupata ugonjwa huu na kumweleza jirani yangu, alighuria kwingine kwa hofu ya kukufa ajaponikaribia. Wauguzi wenzangu ndio walinitembelea na kunijulia hali mpaka nilipopata nafuu. Kutoihisi ladha ya vitu na kutoweza kunusa hiyo ndiyo ishara kamili kuwa una ugonjwa huu wa Covid-19,” akasema.

Caroline Wangui, alikuwa akijichumia riziki kama mhudumu wa Chefs Grill kabla janga la corona kufika nchini. Baada ya serikali kusitisha usafiri wa watu, wakuu wa hoteli hii waliifunga huku ikinilazimu kurejea nyumbani. Hoteli hii ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa misingi ya ushirikiano kati ya Mkenya na Mturuki, bado imefungwa hata wa leo. “Kufutwa kwangu kazini kulinilazimisha kubadilisha mengi maishani. Matumizi yangu ya akiba niliyoweka yalilenga tu mambo muhimu ya maisha. Isitoshe hata sasa bado tasnia hii ya hoteli na utalii inaugumu wake huku ikiwa ngumu kupata ajira,” akasema Wangui.

Centrine Wekesa, mwanamke anayeuza mboga alieleza Taifa Leo Dijitali kuwa baada ya kafyu ya haswa ile ya asubuhi saa kumi na moja hadi saa moja usiku, iliathiri biashara yake sana. “Kikawaida kabla ya ugonjwa huu wa Covid-19, mimi huwapata wateja wengi kutoka saa moja usiku kwani hayo ndiyo masaa ya watu kutafuta cha kununua kwa minajili ya kupika chajio. Wakati ambao kafyu iliwekwa, mauzo ya biashara yangu yalikwenda chini kwani kabla wateja wangu kurekebisha nyakati za kuja kununua. Isitoshe, wengi wa hawa wateja hawakutaka kununua bidhaa zile ambazo walikuwa wananunua awali kwa kuhofia usambazaji wa ugonjwa huu. Hali kadhalika, sokoni kulikuwa na changamoto kwani hukuweza kuchagua bidhaa utakazo kiasi cha kwamba muuzaji alikuwa akikuchagulia na hata kukuwekea bidhaa zilizoharibika huku ikikufanya kuenda hasara kwani singeweza kuuza bidhaa mbovu,” akaeleza Wekesa.

Koporo Odhiambo wa kituo cha polisi cha Daystar alieleza Taifa Leo Dijitali kuwa wananchi huwa na hulka ya kukaidi amri haswa amri hizi zinapotolewa. Wakati rais aliweka kafyu na akasitisha usafiri wa watu kikaunti, wananchi kwa ile hali yao ya kawaida waliikaidi amri na sisi kama polisi ikatulazimu kuhakikisha kuwa amri hii imetekelezwa ipasavyo. Kwa hivyo, nilihakikisha kuwa nimewakumbusha wanabiashara haswa kuzifunga biashara zao kwa wakati unaofaa ili kuepukana na mvutano kati yao na sisi. “Kama watoto wadogo kukumbushwa kila mara cha kufanya sawa sawa wananchi. Isitoshe ni jukumu langu kama askari kuhakikisha kuwa kanuni na sheria za nchi zimekadiriwa kulingana na amri ninazopokea.”

Billy Gacheru, dereva wa masafa marefu wa kampuni ya utengenezaji wa pombe nchini Kenya (KBL) anaeleza Taifa Leo kuwa baada ya janga la corona kufika Kenya na mikakati kuwekwa na serikali kupitia wizara ya afya, hali haikuwa shwari kwao. Hii ni baada ya hata baa na mahali pa kuburudishwa kufungwa.”Kufungwa kwa baa haswa kuliniathiri kiasi cha kuiacha kazi ya usafirishaji wa vileo na kuchukulia kazi ya usafirishaji wa bidhaa zingine. Hata ingawa niliweza kuzisafirisha bidhaa hizi kaunti moja hadi nyingine sababu ya ile barua tuliyopewa sisi kama madereva wa masafa marefu, changamoto ilikuja wakati wa kuvuka mpaka. Ilikulazimu kuwa na barua kutoka nchi zote ilhali kuipata barua hii ilikulazimu kungoja siku mbili kabla ya kuipata. Kusafiri kutoka Kenya hadi Uganda hunichukua siku tatu lakini baada ya masharti ya wizara ya afya, kusafiri huku kunanichukua wiki zaidi ya moja. Kuchelewa huku kulinifanya kutopata pesa kama awali,” akaeleza Bw Gacheru.

You can share this post!

Mama njugu achapa kazi bungeni

Harambee Stars yazamia maandalizi ya mechi ya Sudan Kusini,...