• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Tottenham sasa guu moja ndani ya robo-fainali za Europa League baada ya kupepeta Dinamo Zagreb katika mkondo wa kwanza

Tottenham sasa guu moja ndani ya robo-fainali za Europa League baada ya kupepeta Dinamo Zagreb katika mkondo wa kwanza

Na MASHIRIKA

FOWADI Harry Kane alifunga mabao mawili na kuwasaidia Tottenham Hotspur kupepeta Dinamo Zagreb ya Croatia 2-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Europa League mnamo Machi 11, 2021.

Kane ambaye pia ni nahodha wa Tottenham, aliwafungulia waajiri wake ukurasa wa magoli katika dakika ya 25 kabla ya kucheka na nyavu za wageni wao kwa mara nyingine katika dakika ya 70.

Nusura sogora huyo raia wa Uingereza afunge goli la tatu katika mchuano huo kabla ya kuondolewa uwanjani kutokana na jeraha la goti mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ni matarajio makuu ya kocha Jose Mourinho kwamba Kane atakuwa amepona kiasi cha kuongoza safu ya mbele wakati wa gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Arsenal mnamo Machi 14, 2021 uwanjani Emirates.

“Mchuano ujao wa EPL ni mojawapo ya mechi ambazo kila mwanasoka angependa acheze. Ni matumaini yangu kwamba Kane atakuwa amerejea katika hali shwari kufikia wakati huo,” akasema kocha huyo raia wa Ureno.

Mourinho alikifanyia kikosi alichokitegemea dhidi ya Crystal Palace katika mechi ya awali mabadiliko saba, ila akamdumisha Kane ambaye ushirikiano wake na Gareth Bale na Son Heung-min unazidi kuhisika pakubwa kambini mwa Tottenham.

Kwa kuwa matumaini ya Tottenham kukamilisha kampeni za msimu huu wa EPL ndani ya mduara wa nne-bora na hatimaye kufuzu kwa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao yanazidi kudidimia, Mourinho ameshikilia kwamba fursa kubwa waliyonayo ya kufuzu kwa soka ya UEFA ni kushinda taji la Europa League muhula huu.

Mourinho amewahi kunyanyua taji la Europa League akidhibiti mikoba ya FC Porto nchini Ureno na Manchester United nchini Uingereza.

Bao la kwanza lililofumwa wavuni na Kane lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Erik Lamela aliyepata pia nafasi nyingi za kufunga baada ya kupokezwa krosi kadhaa na Tanguy Ndombele.

Goli la pili ambalo Kane aliwafungia waajiri wake lilitokana na masihara ya beki Kevin Theophile-Catherine aliyeshindwa kuondoa mpira katika eneo la hatari na kumpa Kane fursa ya kumwacha hoi kipa Dominik Livakovic.

Tottenham kwa sasa wamesonga mbele zaidi ya hatua ya 16-bora ya Europa League chini ya kipindi cha misimu mitatu iliyopita baada ya kushinda mechi zote za mikondo ya kwanza dhidi ya Olympique Lyon ya Ufaransa, Inter Milan ya Italia na Wolfsberger ya Austria.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Arsenal pazuri kusonga mbele kwenye Europa League baada ya...

Kiongozi mwenye nia njema afaa kurithi mikoba ya Rais...