• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Matiang’i atoa agizo mitandao ya utapeli ivunjwe sekta ya chai

Matiang’i atoa agizo mitandao ya utapeli ivunjwe sekta ya chai

Na MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i Alhamisi aliwaelekeza maafisa katika kamati za usalama mashinani kunakokuzwa majanichai wazindue mkakati rasmi wa kusaidia wakulima kutimua mitandao ya matapeli kutoka sekta hiyo.

Dkt Matiang’i alisema hiyo ni amri ambayo inafuatia makataa ya Rais Uhuru Kenyatta kutaka wakulima wa majanichai katika vituo vyao vya ushirika na uuzaji wasaidiwe kuandaa chaguzi na wahakikishe kuwa wale ambao wanapendelewa na wengi wa wazalishaji hao ndio wamechukua hatamu za uongozi.

Alizitaka kamati hizo kuandaa mikakati ya kutambua vigogo wa mitandao hiyo ya utapeli ili wazimwe kuwania nyadhifa, na wakiwania, ihakikishwe wameshindwa.

Akiongea mjini Kangari ambapo alizindua ujenzi wa soko la kisasa ambalo litagharimu Sh320 milioni, Dkt Matiang’i alisema kuwa kwa miaka mingi sasa sekta ya majanichai imekuwa chini ya mitandao ya utapeli na wizi na ambapo wakulima wamekuwa wakipoteza zaidi ya Sh10 bilioni kwa mwaka.

Aidha, wakulima wamekuwa wakitoa malalamiko kuwa usimamizi katika shirika lao la KTDA umegeuka kuwa wa unyanyasaji na ndipo serikali ikisaka mbinu ya kuwasaidia wajikomboe, Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya alizindua harakati za kupiga msasa sheria za usimamizi wa sekta hiyo na ambapo aliandaa marekebisho ambayo tayari yametiwa sahihi na Rais na kuwa sheria.

Lakini usimamizi wa KTDA umekuwa ukipinga kwa dhati mabadiliko hayo ambayo Bw Munya anasisitiza kuwa yanalenga kuimarisha pato kwa mkulima kwa zaidi ya asilimia 60.

Naye Dkt Matiang’i mnamo Alhamisi akaweka suala hili wazi.

“Hawa watu wanaojifanya kuwa serikali ya sekta ya majanichai wamekuwa wakihujumu mpango huu wa serikali wa kuweka pesa kwenye mifuko ya wakulima. Nawaagiza wote katika kamati za usalama katika maeneo ya ukuzaji majanichai kuzindua mikakati maalum ya kuwatimua matapeli wote kutoka sekta hii, Na sitaki kusikia vijisababu kuwa haiwezekani, kwa kuwa hiyo ni amri ya Rais Kenyatta,” akasema waziri Matiang’i.

Akionekana kumlenga moja kwa moja mwenyekiti wa sasa wa KTDA Bw Peter Kanyago ambaye amekuwa katika hatamu za uongozi kwa miaka 26 mfululizo sasa, Dkt Matiang’i alikejeli kuwa “huwezi ukashikilia wadhifa wa uongozi hadi mauti yakutimue. Hivi vyeo vya uongozi huwa ni vya muda na inafaa ukiongoza kwa muda unaostahili unaondoka na wengine waendeleze mbele hiyo kazi.”

Alifafanua kuhusu amri yake, Dkt Matiang’i alisema maafisa wa usalama wanafaa wachukue udhibiti wa kusaidia wakulima hao wasiviziwe na mitandao hiyo ambayo huwa na mazoea ya kuandaa chaguzi bandia katika hoteli na hatimaye kukimbia mahakamani kulinda orodha ya waliopendekezwa kuongoza wasitimuliwe ama na wakulima au na serikali.

Hatimaye, wakulima hujipata wakitozwa ada za ziada za kugharimia kesi hizo mahakamani na katika hali hiyo, kilio kuzidi kutanda kuhusu malipo duni na bonasi ambazo kwa mfano, zimekuwa zikipoteza Sh10 kwa kila mwaka kwa miaka 10 sasa ikifuatana.

Dkt Matiang’i alisema kuwa hataki kusikia akiambiwa kuwa mitandao hiyo iliyokita mizizi katika sekta za kilimo na ambapo hupunguza pato kwa wakulima, kwamba “haiwezi ikatimuliwa.”

“Sisi ni serikali na ikiwa lengo ni kumfaa mkulima apate haki ya jasho lake, sitaki kusikia vijisababu. Hii ni kazi ambayo ni lazima tuifanye na itafanyika,” akasema.

You can share this post!

Zack Kinuthia afichua kuhusu mpango wa Sh5.6 bilioni kukuza...

Kagame ndiye kiongozi wa kwanza Afrika Mashariki kupata...