• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Matiang’i asisitiza haja ya mahakama, DCI na DPP kushirikiana katika utendakazi

Matiang’i asisitiza haja ya mahakama, DCI na DPP kushirikiana katika utendakazi

Na SAMMY WAWERU

KESI zinazowasilishwa kortini haki itapatikana endapo Idara ya Mahakama, Uchunguzi wa Jinai (DCI) na Mashtaka ya Umma (DPP) zitashirikiana katika utendakazi, amesema Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i.

Dkt Matiang’i amesema Ijumaa kinachosababisha haki kukosekana na kesi kutupiliwa mbali, ni asasi hizo kukosa kushirikiana.

“Tutakaposhirikiana tutafanya kazi vizuri na kuenda mbali,” akasema waziri huyo.

Alisema hayo katika hafla ya kufuzu na kutuza maafisa kadha wa mashtaka ya umma, baada ya kupitia mafunzo kuimarisha utendakazi wao.

Kauli ya Dkt Matiang’i imejiri siku chache baada ya kunyooshea kidole cha lawama idara ya mahakama, akilalamikia imelemaza vita dhidi ya uhalifu na ufisadi nchini kufuatia kucheleweshwa kwa usikilizaji wa kesi na pia kufanya maamuzi.

Waziri Matiang’i alieleza kushangazwa kwake na jinsi kesi zinavyokawishwa kortini, utepetevu aliotaja umechangia haki kutopatikana kwa waathiriwa.

Alitumia mfano wa wanasiasa wanaokamatwa kwa kuchochea ghasia na vurugu wakati wa chaguzi, walanguzi wa dawa za kulevya na pia majangili, akisema kesi zao huchukua miaka mingi kusikilizwa na kuamuliwa, jambo ambalo husababisha kesi hizo kufutiliwa mbali.

“Asasi zetu za uchunguzi na kusikiliza kesi zikiwa duni, hatutapata matokeo bora. Idara ya mahakama, DCI na DPP zikichakachuliwa haki haitapatikana,” Dkt Matiang’i akasema, akihimiza haja ya ushirikiano ili kuboresha kazi.

Idara ya mahakama imekuwa ikilalamikia upungufu wa raslimali za kutosha na pia fedha kuendesha kazi.

You can share this post!

Timu kubwa Kenya zaumia kutokana na ukosefu wa viwanja

Rais azima mikutano mikubwa ya kisiasa kwa siku 30