• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
TAHARIRI: Uamuzi wa kafyu uzingatie usalama

TAHARIRI: Uamuzi wa kafyu uzingatie usalama

KITENGO CHA UHARIRI

LEO Rais Uhuru Kenyatta ana kibarua kigumu.

Anatarajiwa afanye uamuzi wa iwapo atawaridhisha wafanyabiashara wanaolia kupata hasara sababu ya kafyu, au aendeleze marufuku na kulinda maisha ya wananchi.

Wakenya wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa Rais amalize marufuku ya watu kutoka nje kati ya saa nne na saa kumi za usiku.

Wanaopigania kafyu iishe, wanasema hakuna dalili kwamba corona itaisha hivi karibuni. Kwamba kilicho muhimu ni wananchi wajifunze kuendelea kuzingatia kanuni kuu za kunawa mikono, kuvaa barakoa na kutogusa pua, midomo na macho.

Ingawa viwango vya maambukizi vimeanza kupanda tena, kupatikana kwa chanjo kunaleta matumaini. Serikali imepata chanjo ya AstraZeneca kutoka India na Sputnik V kutoka Urusi.

Chanjo hizi kwa sasa zitatolewa kwa watu walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa. Hao ni watoaji huduma muhimu ambazo huwalazimu kutangamana na watu wengi kama walimu, wahudumu wa afya, magavana na kadhalika.

Uamuzi wa kuendeleza au kumaliza kafyu si jambo la kufanywa bila kutafakari faida na hasara.

Ni kweli wafanyabiashara huchelewesha bidhaa zao kwa kuwa wao wenyewe hawaruhusiwi kutembea usiku. Lakini magari ya kusafirisha bidhaa yana vibali. Wanaotaka kafyu imalizike hawajaeleza kama wanakatazwa kusafirisha bidhaa zao kupitia magari hayo.

Uamuzi wowote atakaochukua Rais, jambo muhimu kwetu ni kuzingatia kanuni ambazo Rais Kenyatta mwenyewe alizitangaza awali lakini zimepuuzwa na wanasiasa.

Kiini kikubwa cha usambazaji virusi vya corona ni mikutano ya kisiasa. Tunafahamu kwamba kuna kampeni ya kupigia debe mswada wa BBI na kampeni za uchaguzi mdogo wa Machakos, Garissa na Bonchari zinaendelea.

Mikusanyiko hii yafaa kusimamishwa mara moja, na wananchi na viongozi washurutishwe kutii maagizo ya kutotangamana kwenye mikusanyiko ya zaidi ya watu 200.

Wanasiasa yafaa washauriwe kuja na mbinu za kisasa za kuwafikia watu wengi bila ya kukusanyika. Kampuni na mashirika mengi yanaendeleza shughuli kupitia mitandao, Zoom, WhatsApp, Facebook, YouTube na kadhalika.

Kuna wakati tulipokaribia kufanikiwa kuangamiza corona lakini mapuuza ya viongozi yameturudisha pabaya.

You can share this post!

Rangers na Slavia nguvu sawa katika mkondo wa kwanza Europa...

Arsenal pazuri kusonga mbele kwenye Europa League baada ya...