• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
OMAUYA: Handisheki isigeuzwe kisa cha nyani na mbwa

OMAUYA: Handisheki isigeuzwe kisa cha nyani na mbwa

Na MAUYA OMAUYA

NI miaka mitatu tangu handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ilipotokomeza uhasama na mzozo wa kisiasa uliotishia kuvuruga amani, kuzua migawanyiko ya kikabila na kusambaratisha umoja wa taifa tunaloliita Kenya.

Ikumbukwe kwamba katika kilele cha mzozo huo wa kisiasa, majimbo kadhaa yalinuia kujitenga na kudinda kuchangia hata ushuru kwa serikali ya kitaifa.

Wakati huo huo kwa kinyongo na hamaki vikosi vya polisi vilitii amri ya kuwazima wapinzani kwa makali ya mtutu wa bunduki.

Damu ilimwagika na simanzi ikatanda. Raia wengi walisusia bidhaa na huduma za mashirika fulani na hali hii ingeendelea kwa miezi zaidi, nchi hii ingechanikachanika kiuchumi na kiutawala.

Handisheki ilileta utulivu na ikazaa ahadi ya utaifa mpya.

Miaka mitatu baadaye, yawezekana kumbukumbu ya 2017 imeanza kuyeyuka kutoka kwenye mawazo ya Wakenya.

Dhamira ya handisheki imegeuzwa kuwa miereka ya mibabe wa siasa na ahadi ya BBI kuwa kinyang’anyiro cha ubinafsi.

Mapatano ya Raila na Uhuru si ahadi ya maharusi wawili wanaoelekea fungate.

Mapatano haya yalikomesha machafuko na kuokoa jahazi la raia milioni 47 lililokuwa linaenda mrama kwa mawimbi ya siasa chafu.

Tutajuta kama taifa iwapo tutageuza handisheki kuwa kisa cha nyani na mbwa.

Nyani na mbwa walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Waliitana ‘ndugu’ na kufaana kwa kila jambo; ulimi na mate.

Siku moja walialikwa kwenye karamu na wakaamua hii ndiyo bahati yao ya kupata posa na ndoa. Nyani alipendekeza wajirembeshe na kujikwatua ili wapendeze vilivyo.

Mbwa alifurahia mno wazo hili na akamnyoa nyani nywele na malaika kwa ustadi mkubwa.

Alimtengeneza kwa uangalifu, akampamba kwa michoro usoni na mwilini.

Baadaye akamkata kucha miguuni na mikononi kabla ya kumchagulia mapambo murua ya kuvutia; vipuli, herini, wanja, rangi ya midomoni. Wah! Nyani alipambwa akapambika.

Kisha akamtia marashi yaliyonukia ajabu. Nyani alipojitazama katika kioo hakuamini urembo wake. Alipendeza hakika.

Nyani alipochukua usukani kumpamba mwenzake aliwaza jinsi ingekuwa iwapo angevutia warembo wote na kuzoa sifa zote kwenye karamu.

Japo alikuwa kinyozi hodari, wivu ulimtawala nyani. Basi alianza kwa kumduwaza mbwa kwa wimbo mtamu.

Mbwa alijibwaga kwa starehe ya wimbo, usingizi ukamteka, basi hakutazama jinsi alivyotengenezwa.

Pindi tu alipogutuka, mbwa hakuamini macho yake alichokiona katika kioo.

Mwenzake alikuwa amemuumbua na sura yake ikawa mbaya na ya kuchukiza; jinsi alivyo hadi sasa.

Alijitazama tena kiooni akasikitika na kwa hamaki akaapa kulipiza kisasi.

Mbwa alimrukia kwa hasira, lakini nyani akaponyoka na kukwea mtini kuepuka meno ya mbwa.

Mbwa alimwandama hadi kwenye shina, akabaki chini ya mti akifoka kwa hasira, “Pita juu nami nitapita chini”.

Kwa sababu ya tamaa, wivu na roho ya usaliti, urafiki wa nyani na mbwa uliangamia na kutia vizazi vyao katika uadui unaodumu hadi leo.

Hii ndiyo njia panda inayowakabili Raila na Uhuru hasa kufuatia wiki iliyojaa malumbano ya usaliti kutoka kwa wafuasi wao.

Mahasidi wanaoemezea mate kuvunjika kwa handisheki ni wale wanaotazama mapatano hayo kwa darubini ya uchaguzi wa 2022 na maslahi ya vigogo hao pekee.

Zaidi ya kisa cha nyani na mbwa ikumbukwe kwamba taifa hili linahitaji ukomavu wa demokrasia na maridhiano ya kweli ili kuondoa uhasama wa kihistoria unaolipuka kila wakati wa uchaguzi.

Ikiwa handisheki itazama, hakika tutakuwa tumerejesha taifa hili katika vichaka vya miaka ya 1960 na kuamsha hisia za uonevu ambazo zimedhuru uhusiano wa kikabila hadi sasa.

Hatari itakayoibuka haitadhuru Raila na Uhuru pekee. Wasafiri ni wengi kwenye chommbo cha handisheki! Manahodha yatakiwa wawe macho!

[email protected]

You can share this post!

Aliyefutwa sababu ya ujauzito atuzwa Sh1.4m

MATHEKA: Wanasiasa wamechangia wimbi hili la tatu la corona...