• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
MATHEKA: Wanasiasa wamechangia wimbi hili la tatu la corona nchini

MATHEKA: Wanasiasa wamechangia wimbi hili la tatu la corona nchini

Na BENSON MATHEKA

KWA muda wa majuma mawili yaliyopita, idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imekuwa ikiongezeka, hali iliyowafanya wataalamu kuonya kuwa kuna wimbi la tatu la mkurupuko wa janga hilo humu nchini.

Hii inajiri wakati ambao wataalamu wameonya kwamba kuna uwezekano wa aina mpya ya virusi hivyo nchini.

Ni tukio linalojiri miezi mitatu baada ya shule kufunguliwa.

Kuanzia Disemba mwaka jana, serikali ililegeza masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo baada ya uchumi kudorora na watu wengi hasa maskini kuteseka.

Wakati huo serikali ilikuwa ikikabiliwa na wakati mgumu wala haikuwa na budi ila kufungua uchumi kuokoa maisha ya watu huku ikiwataka raia kuwajibika kuepuka mkumbo wa tatu wa maambukizi.

Hata hivyo, viongozi na maafisa wakuu serikalini na wanasiasa ambao walipaswa kuwa katika mstari wa mbele kuonyesha mfano mwema kwa kufuata kanuni za wizara ya Afya za kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, walizipuuza kanuni na kuandaa mikutano mikubwa ya kisiasa kupigia debe mswada wa kubadilisha katiba na kuendeleza siasa za urithi katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Wananchi nao waliwaiga viongozi na maafisa hao na kuacha kuzingatia kanuni za wizara za Afya katika shughuli zao za kila siku.

Kufuatia tabia hii, wataalamu wa afya walionya kwamba kulikuwa na hatari ya maambukizi ya corona kuongezeka Machi, ubashiri ambao umeanza kutimia huku kiwango cha maambukizi kikiongezeka kutoka asilimia mbili wiki za kwanza za Februari hadi asilimia 13 katika wiki ya kwanza ya Machi.

Matokeo yamekuwa ni hospitali kuanza kulemewa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji hewa ya oksijeni kuwasaidia kupumua na kuna hofu hali inaweza kuwa mbaya zaidi ikithibitishwa kuwa kuna aina mpya ya virusi hivyo nchini.

Kama wanasiasa na maafisa wakuu wa serikali wangetii maagizo ya wizara ya Afya na kuonyesha mfano, huenda Kenya ingeepuka hali inayoshuhudiwa kwa wakati huu na uchumi kufunguliwa kikamilifu.

Hata hivyo, inasikitisha hata magavana wa kaunti wanaopaswa kuhakikisha kaunti zao zina vituo vya kutenga na kutibu wanaoambukizwa virusi vya corona walikuwa miongoni mwa viongozi waliopuuza kanuni za wizara hiyo.

Kwa sababu ya mapuuza ya viongozi na Wakenya wanaoabudu wanasiasa na vitendo vyao, kuna hatari ya virusi hivyo kusababisha hasara kubwa kwa maisha ya watu na uchumi wa nchi.

You can share this post!

OMAUYA: Handisheki isigeuzwe kisa cha nyani na mbwa

Mbunge ajipata pabaya kwa kutaka kuzima wapenzi wa nje ya...