• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Corona: DP Ruto asitisha mikutano yake ya hadhara

Corona: DP Ruto asitisha mikutano yake ya hadhara

Na CHARLES WASONGA

SAA chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na ya kijamii kwa siku 30, Naibu Rais William Ruto amesitisha mikutano yake yote ya hadhara aliyokuwa ameratibu sehemu mbalimbali nchini.

Kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter Dkt Ruto alisema amechukua hatua hiyo kwa heshima ya marufuku yaliyotangazwa kwa lengo la kuzuia maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Dkt Ruto amekuwa akizuru sehemu mbalimbali nchini kujinadi kwa wananchi kuhusiana na ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

Ruto pia amekuwa akinadi vuguvugu lake la hasla kama linalotetea walala hoi.

Amesema Ijumaa mlipuko wa wimbi la tatu la maambukizi ndicho kiini cha serikali kuchukua hatua kama hiyo.

“Ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 limeibua hofu kubwa nchini ndiposa serikali ikaamua kuweka masharti zaidi ya kudhibiti janga hili,” akasema Dkt Ruto.

“Kufuatia hatua ya Rais kutangaza masharti hayo ya kuzuia maambukizi ya corona, nimesimamisha mikutano yangu yote ya umma hadi wakati usiojulikana,” akaongeza.

Kwenye hotuba ya kitaifa kuhusu hali ya Covid-19 nchini aliyoitoa katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta alipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa na kijamii kwa siku 30 kuanzia Ijumaa Machi 12, 2021 usiku wa manane.

Vile vile, Rais aliamuru kwamba hafla za mazishi zitakuwa zikihudhuriwa na watu 100, watu wa familia ya mwendazake.

Vile vile, kiongozi wa taifa ameagiza makanisa na vyumba vingine vya ibada viruhusu thuluthi moja pekee ya waumini kwa wakati mmoja, miongoni mwa masharti mengine.

You can share this post!

Mwanaspoti wa Safari Rally azikwa

Madereva tayari kupaisha mashine zao kuwania alama kwenye...