• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Vinara wa EPL wanataka mashabiki 10,000 kuruhusiwa viwanjani kuhudhuria mechi mbili za mwisho wa msimu huu wa 2020-21

Vinara wa EPL wanataka mashabiki 10,000 kuruhusiwa viwanjani kuhudhuria mechi mbili za mwisho wa msimu huu wa 2020-21

Na MASHIRIKA

VINARA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wana mipango ya kuhakikisha kwamba mashabiki watahudhuria mechi za raundi mbili za mwisho za kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Haya ni kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa EPL, Richard Masters.

Kwa mujibu wa kinara huyo, mashabiki kufikia 10,000 wataruhusiwa uwanjani kuhudhuria mechi za EPL zitakazosakatwa kuanzia Jumatatu ya Mei 17 iwapo serikali ya Uingereza itadumisha mikakati iliyopo kwa sasa katika juhudi za kukabiliana na maambukizi mapya ya Covid-19.

Ili kuhakikisha kwamba viwango vya ushindani vinasawazishwa, vikosi vyote 20 vya EPL vitasakata angalau mechi moja kati ya mbili za mwisho wa msimu huu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Ili kufanikisha hilo, basi italazimu mechi zilizopangiwa awali kusakatwa kati ya Mei 18-20 kuratibiwa upya kabla ya mechi za raundi ya mwisho kuchezwa Mei 23, 2021.

“Tuna imani kwamba mechi za raundi mbili za mwisho zitahudhuriwa na hadi mashabiki 10,000 wa kila kikosi nyumbani kwao. Hiyo itakuwa nzia nzuri zaidi ya kukamilisha kampeni za muhula huu wa 2020-21 na kuwapa mashabiki angalau kitu cha kujivunia zaidi,” akasema Masters.

Katika juhudi za kufanikisha mipangilio hiyo, Masters amedokeza kuhusu uwezekano wa mechi za raundi ya 36 kuhamishwa kutoka Jumanne ya Mei 11 na Jumatano ya Mei 12 hadi wiki inayofuata.

Hata hivyo, lipo pendekezo jingine la kuhamisha mechi zote za raundi ya 36 hadi wikendi inayofuata japo hatua hiyo italeta mgongano wa ratiba ikizingatiwa kwamba fainali ya Kombe la FA imepangwa kufanyika Mei 15, 2021.

Marejeo ya mashabiki uwanjani yataleta matumaini tele katika msimu ambao umekuwa mgumu zaidi kwa vikosi vyote vya EPL ambayo vilitandaza pia robo ya mwisho ya kampeni za muhula wa 2019-20 bila mashabiki viwanjani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TANZIA: Mwanamuziki Muriithi John Walker afariki baada ya...

Wanaofariki kuzikwa chini ya saa 72