• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Watanzania waulizia aliko rais huku serikali ikinyamaza

Watanzania waulizia aliko rais huku serikali ikinyamaza

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, Tanzania

SERIKALI ya Tanzania imeendelea kunyamaza huku raia wakiuliza aliko rais wao John Magufuli anayedaiwa kuugua corona.

Badala ya kueleza aliko rais huyo, maafisa wa serikali wameonya wanahabari na raia dhidi ya kuandika na kusambaza habari wakishuku aliko kiongozi wa nchi yao na hali yake ya afya. Maafisa wa serikali pia wametishia kumchukulia hatua kiongozi wa upinzani Tundu Lissu anayeishi uhamishoni Ubelgiji kwa kudai kwamba Magufuli alipelekwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kuugua.

Bw Lissu anadai kwamba Bw Magufuli alilazwa katika Nairobi Hospital jijini Nairobi, Kenya Jumatano akiugua virusi vya corona.

Kupitia ujumbe wa Twitter, Bw Lissu alisema kwamba Magufuli ambaye alikataa kuweka kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona nchini Tanzania alilazwa katika hospitali moja jijini Dar es Salaam, kabla ya kuhamishiwa Nairobi hali yake ya afya ilipodorora.

Ingawa Nairobi Hospital ilikataa kukanusha au kuthibitisha iwapo rais huyo amelazwa humo, usalama uliimarishwa kuanzia Jumanne huku wageni wakizuiwa kutembelea eneo la North Wing lililo na wodi za kulazwa watu mashuhuri.

Mnamo Alhamisi, Bw Lissu alisema kwamba alidokezewa rais huyo alihamishiwa India. Hata hivyo, duru nyingine zilisema kwamba kiongozi huyo anatumia mashini kumsaidia kupumua na katika hali hiyo, madaktari hawawezi kumruhusu kusafiri hadi India.

“Wanapanga kumpeleka India kwa siri kuepuka kuaibishwa na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii. Wanahisi kwamba itakuwa aibu iwapo kibaya zaidi kinaweza kutendeka Kenya. Mtu mwenye nguvu zaidi Tanzania anaondolewa kwa siri kama mhalifu,” Lissu aliandika kwenye Twitter.

Duru zilisema kwamba rais huyo hajaonekana hadharani tangu Februari 27.

Bw Lissu aliambia shirika la habari la BBC kwamba kimya cha serikali kinafanya wengi kueneza uvumi kwa kuwa afya ya rais haifai kuwa suala lake la kibinafsi.

Ijumaa, waziri wa habari wa Tanzania, Innocent Bashungwa, alionya wanahabari nchini humo dhidi ya kueneza uvumi kuhusu aliko Magufuli.

Aliwataka wanahabari kuandika habari zilizothibitishwa na maafisa wa serikali wanaohusika.

“Natoa wito kwa wanahabari na wananchi wetu kuendelea na utaratibu wa kupata taarifa kupitia vyanzo rasmi vya habari. Kutumia uvumi kama habari rasmi ni kukiuka sheria zinazosimamia sekta ya habari. Epukeni kusambaza habari ambazo mtawajibika nazo,” alisema kupitia Twitter.

Inasemekana kuwa maafisa wengine kadhaa wa serikali ya Magufuli wamelazwa Nairobi Hospital wakiwa na dalili za ugonjwa wa corona.Bw Magufuli hajaonekana hadharani kwa siku 12. Alikosa kuhudhuria mkutano wa marais wan chi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na badala yake akawakilishwa na makamu wake Samia Suluhu.

You can share this post!

Chanjo: Rais aondoa hofu kuhusu AstraZeneca

Watolewa hospitalini na kuuawa na umati