• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
TAHARIRI: Klabu za ‘kikabila’ zitastawisha soka

TAHARIRI: Klabu za ‘kikabila’ zitastawisha soka

KITENGO CHA UHARIRI

HAIPINGIKI kwamba klabu za AFC Leopards na Gor Mahia ndizo zenye mashabiki wengi zaidi nchini.

Mbali na klabu hizo, nyingine inayopendwa zaidi ni Bandari FC yenye makao yake jijini Mombasa. Hii hupendwa kwa sababu Wapwani huiona kama milki yao.

Kinyume na ukweli huo, klabu zenye uwezo na ufanisi mkubwa kama vile Tusker, Ulinzi Stars na hata Mathare United, licha ya kwamba zimekuwapo kwa muda mrefu, hazina mashabiki wa kuridhisha kwa idadi. Zinapocheza, huwa nadra sana kuwapata mashabiki wafikao 1,000 uwanjani wakizishabikia klabu hizo ambazo nyingi hudhaminiwa hasa na mashirika ya kibiashara.

Ili mpira kukua kama ilivyo nchini Uingereza, Uhispania, Ufaransa, Italia na hata Ujerumani ambapo timu yoyote inapocheza hata ziwe zile klabu ndogongogo, watu hufurika hadi pamoni viwanjani, sharti mikakati ibuniwe ambapo klabu zote za Kenya zitapata ushabiki mwingi.

Vinginevyo, kandanda ya Kenya itabakia tu hapo ilipo au ustawi wake uwe wa mwendo wa aste aste zaidi.

Mashabiki ni muhimu uwanjani kwa kuwa wanapojazana ugani timu zinapocheza, timu hizo hupata pesa za kiingilio. Pesa hizo huzisaidia klabu hizo kujiendeleza kwa kulipa wachezaji na maafisa wake mshahara bila kutegemea udhamini pekee.

Hatumaanishi kuwa sasa wadhamini wasitoe ufadhili kwa timu hizi; la hasha. Udhamini ni muhimu maana unaziwezesha klabu hizo kupata pesa nyingi kwa wakati mmoja na tena mapema hivyo basi kuzisaidia kuweka mipango imara.

Hata hivyo, mashabiki ni muhimu kwa sababu mbali na kutoa kiingilio kwa faida ya klabu, pia hunogesha mpira kutokana na hekaheka zao wawapo uwanjani.

Je, mbinu gani itumiwe kufanikisha uwepo wa klabu nyingi za kikabila kama vile Gor inayoshabikiwa kwa wingi na Wakenya wanaotoka Nyanza na Leopards inayopendwa na watu wa Magharibi?

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lafaa libuni mbinu za kuzikuza klabu za kijamii kwa mfano Mumbi United ya eneo la Kati, Musyii ya Ukambani, Gusii au Shabana ya Gusi, Chamge Rangers ya Rift Valley na kadhalika.

FKF inaweza kufanikisha hilo kwa kuzipigania klabu za aina hii kupata udhamini kutoka kwa mashirika ya kibiashara kama vile Safaricom, Equity Bank, KCB na kadhalika.

You can share this post!

Watolewa hospitalini na kuuawa na umati

MUTUA: Hivi tunaweza kujilisha au tunaringa bure tu?