• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KAMAU: Serikali isaidie HELB kutoa mikopo upesi kwa wanafunzi

KAMAU: Serikali isaidie HELB kutoa mikopo upesi kwa wanafunzi

Na WANDERI KAMAU

VIJANA ndio msingi wa mustakabali wa taifa lolote duniani.

Bila uwepo wa vijana, jamii huwa kama nyumba iliyojaa giza totoro.

Vijana ndio injini ya ufanisi wa jamii husika katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Ni sababu hiyo ambapo nchi nyingi duniani huwa zinatilia mkazo masuala yanayohusu maslahi ya vijana, hasa elimu, sayansi na teknolojia.

Tathmini pevu ya kihistoria inaonyesha kuwa jamii nyingi zinazowekeza kwenye vijana hupata ufanisi mkubwa katika nyanja zote muhimu baadaye.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa wakati dunia nzima inasisitiza kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika masuala ya vijana, Kenya inayumba.

Vijana wengi nchini wanaishi kama mateka. Wanaishi kama wakimbizi waliotengwa na kusahaulika na walezi wao. Wanaishi kwa upweke mkubwa unaoandamwa na mahangaiko ya kila siku.

Serikali inaonekana kutojali vilio vyao. Hii ni licha ya serikali iyo hiyo kusisitiza kuwa inajali maisha yao ya baadaye. Wanasalitiwa kila siku huku wakipewa ahadi za maisha ya kifahari na kifalme siku za usoni!

Usaliti huo unadhihirishwa na hatua ya Serikali kuchelewa kuifadhili Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB).

Bodi hiyo ndiyo huwa inatoa mikopo kwa vijana walio kwenye taasisi za elimu ya juu kama vile vyuo vikuu na vile vya kadri, kuwasaidia kulipia karo zao na kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, ucheleweshaji huo umezua ghadhabu kubwa miongoni mwa wanafunzi, hasa katika vyuo vikuu, ambapo baadhi wamejitokeza kueleza masaibu wanayopitia kwa kukosa fedha.

Mnamo Jumatano, wanafunzi hao walifanya maandamano ya amani katika sehemu mbalimbali nchini, wakieleza ni vigumu kuendelea na masomo yao bila fedha za kugharamia mahitaji yao ya msingi.

Katika Chuo Kikuu cha Moi, jijini Eldoret, baadhi walitoa simulizi za kufadhaisha, kuhusu namna wanavyolazimika kukaa chuoni kwa siku kadhaa hata bila kupata chakula!

Simulizi kama hizo ni za kushtua katika nchi ambako serikali imeorodhesha makumi ya mikakati na ajenda za kuboresha maisha ya vijana.

Ni vipi vijana watasoma wakiwa na njaa? Hili haliwezekani hata kidogo.

Hayo ni mazingira magumu kwa wanafunzi hao na nawaunga mkono katika kuishinikiza serikali kuharakisha kwenye utoaji wa fedha hizo.

Taswira hizo ni za kutamausha sana, kwani zinaibua maswali kuhusu ikiwa uongozi uliopo kweli unawajali vijana.

Huu ni usaliti kwao, ambapo lazima wanaohusika wakabiliwe ifaavyo.

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Hivi tunaweza kujilisha au tunaringa bure tu?

FUNGUKA: ‘Si uchizi, ni raha zangu…’