• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
FATAKI: Ubabe-dume, ujeuri na ujuaji mwingi si ujasiri, ni ugumegume

FATAKI: Ubabe-dume, ujeuri na ujuaji mwingi si ujasiri, ni ugumegume

Na PAULINE ONGAJI

WIKI kadha zilizopita bwana mmoja mtandaoni alionekana kuwashangaza wengi alipochapisha ujumbe akimuomba mkewe msamaha kwa kuwa na jicho la pembeni.

Ni suala lililoibua mjadala mkali hasa miongoni mwa baadhi ya wanaume waliodai kuwa hatua yake hiyo ilikuwa ya kipumbavu, huku wengine wakimtaja kuwa dhaifu kwa “kumpigia mwanamke magoti.”

“Tangu lini mwanamume akakiri kosa la ulaghai wa mapenzi hasa hasa kwa mkewe?” bwana mmoja alishangaa!

Kuna wale waliohoji kwamba msamaha unapaswa kuwa wa kisiri. Nakubaliana na hoja hiyo ya usiri lakini ujasiri wa bwana huyo unapaswa kuigwa na baadhi ya wanaume hasa humu nchini wanaofananisha ungwana wa aina hii na udhaifu.

Kuna baadhi ya wanaume ambao katika karne hii ya 21 wanazidi kutawaliwa na taasubi ya kiume kwamba kuomba msamaha kunawapunguzia nguvu na sifa za kiume.

Baadhi ya wanaume hawafahamu uzito wa neno pole hasa katika uhusiano. Tatizo ni kwamba wengi wanazidi kuongozwa na kiburi na kudhani kuwa sifa kama hiyo inawafanya spesheli machoni pa mabinti.

Ni upumbavu huu unaowafanya baadhi yao wasitilie mkazo mambo muhimu katika uhusiano, na ambayo yameonekana kuyeyusha mioyo ya mabinti wengi kama vile kumpisha mjamzito kwenye foleni au hata ndani ya matatu, kumshika mwenzio mkono mnapovuka barabarani au hata kumsaidia katika kazi ndogondogo nyumbani. Badala yake, tunashuhudia tabia za ubabe dume kinyume na enzi za babu zetu waliokuwa wakimlinda mwanamke pasipo kuzingatia uhusiano baina yao.

Lakini tena ukitazama kwa makini utatambua kwamba tabia hii haijakithiri tu miongoni mwa madume wa humu nchini, nikidhani ni suala la kizazi hiki. Na hii ndio pia imefanya mabinti wa sasa kuonekana kana kwamba wameota pembe.

Ikiwa tunataka mabinti wa kisasa warejelee sifa ya kale ya unyenyekevu, basi lazima wanaume nao pia waonyeshe nia ya kuwatunza na kuwalinda, sawa na jinsi mababu zetu walivyowaheshimu wanawake.

Ikiwa hawako tayari kufanya hivyo, basi wajiandae kwa kizazi cha mabinti wasiozingatia heshima na ambao wako tayari kufanya kila wawezalo kujilinda kutokana na ufedhuli wa wanaume wa kizazi cha sasa wasiojua umuhimu wa ustaarabu.

You can share this post!

CHOCHEO: Ukijua anachepuka, utafanyaje?

MWANAMUME KAMILI: Ukipenda ama kupendwa jamani sichezee...