• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
JAMVI: Raila anajitia hatarini kuhepwa ifikapo 2022

JAMVI: Raila anajitia hatarini kuhepwa ifikapo 2022

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, yuko kwenye hatari ya kuachwa mpweke kisiasa ifikapo 2022, kutokana na tofauti ambazo zinaendelea kuibuka baina yake na vigogo wenzake waliokuwa pamoja katika muungano wa NASA.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Odinga amekuwa akijibizana vikali na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kuhusu mkataba waliotia saini kubuni muungano huo.

Tofauti hizo pia zimeongezwa na ushindani mkali ulioibuka kati ya vyama vya ODM na ANC katika eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega majuma mawili yaliyopita, ambapo Bw Peter Nabulindo wa ANC aliibuka mshindi dhidi ya Bw David Were, aliyewania kwa tiketi ya ODM.

Kutokana na matokeo hayo, cheche za maneno zimeongezeka kati ya pande hizo mbili hasa kuhusu ghasia zilizotokea, mrengo wa Bw Odinga ukidai Bw Mudavadi “alipendelewa na serikali.”

Kutokana na mielekeo hiyo, wadadisi wa kisiasa wanaonya kuwa kuna hatari ya Bw Odinga kujipata peke yake kisiasa, ikiwa majibizano hayo yataendelea kushuhudiwa.

Wanasema kuwa hilo linachangiwa na hali kwamba ilivyo sasa, Bw Odinga anaonekana kukwaruzana na kila mwanasiasa.

“Si taswira nzuri wakati kiongozi anatofautiana na karibu kila mwanasiasa mwenye ushawishi. Ni hali inayotia doa na kupunguza uwezekano wowote baina yao kushirikiana,” akasema Bw Javas Bigambo ambaye ni mdadisi wa kisiasa.

Mustakabali wa Bw Odinga kisiasa pia unaelezewa kuhatarishwa na wasiwasi uliopo miongoni mwa washirika wake kuhusu uthabiti wa handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, na uhusiano mbaya ambao umekuwepo kati yake na Naibu Rais William Ruto.

“Washirika wa Bw Odinga wanapaswa kumshauri anyenyekee na aepuke kujibizana na vigogo wenzake. Sababu kuu ni kwamba kando na handisheki, hakuna mrengo mwingine wa kisiasa ambao haujakwaruzana na ODM kuhusu usaliti ama ushirikiano wa kisiasa,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye pia ni mdadisi wa siasa.

Mabwana Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula wameelezea nia ya kuungana, jambo ambalo lilidhihirika katika kampeni za chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai (Bungoma) na Useneta katika Kaunti ya Machakos.

Kwenye kampeni katika eneo la Matungu, Bw Wetang’ula alisema umetimu wakati wa Bw Odinga kuunga mmoja wao kuwania urais pia, kwani “wamemwachia” nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Kama hilo halitoshi, wadadisi pia wanatabiri “kibarua kigumu” kwa Bw Odinga kuendelea kuudhibiti kisiasa ukanda wa Pwani, baada ya baadhi ya viongozi kuanza kushinikiza wenzao kubuni chama huru cha eneo hilo.

Juhudi hizo zinaongozwa na Gavana Amason Kingi wa Kilifi, anayeshikilia kuwa wenyeji wanapaswa kuwa na chama chao cha kisiasa, kama ilivyo katika maeneo mengine nchini.

Hata hivyo, kauli yake imekosolewa vikali na Bw Odinga, anayesema hatua hiyo ni “ya kuirejesha Pwani nyuma kisiasa.”

Ukanda huo umekuwa miongoni mwa ngome kuu za kisiasa za Bw Odinga, ambako ODM ina umaarufu mkubwa.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa za Pwani wanasema kujitokeza kwa viongozi kama Bw Kingi kunaonyesha kwamba wenyeji bado hawajaona faida ya kuendelea kuwa wafuasi wa Bw Odinga.

“Kauli ya Bw Kingi inaonyesha uasi wa kichinichini uliopo dhidi ya ODM na Bw Odinga. Ni ishara ya wazi kuwa wenyeji wanahisi huu ni wakati wao kuwa na chama huru cha kisiasa ambacho kitaendeleza maslahi yao,”asema Prof Halimu Shauri, ambaye ni mdadisi wa siasa za ukanda huo.

Anasema Bw Odinga anafaa aanze kutathmini mwelekeo wake kisiasa, hasa baada ya viongozi wengine kama Gavana Hassan Joho (Mombasa) kutangaza kuwa watawania urais.

“Hizi zote ni ishara kwamba eneo hili limeanza kutathmini jinsi linavyoweza kuendeleza siasa zake lenyewe bila kutegemea miongozo kutoka nje,” asema Prof Shauri.

You can share this post!

JAMVI: Athari ya Uhuru kusema ‘fulani’ tosha

DINI: Msalaba ndio siri ya mafanikio; hakuna utukufu bila...