Raila aondoka hospitalini, kuendelea kujitenga nyumbani

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM ameondoka hospitalini wiki moja baada ya kulazwa kwa kuambukizwa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Waziri huyo mkuu wa zamani Jumapili aliweka video katika akaunti yake ya Twitter akionekana akifanya mazoezi nyumbani kwake katika mtaa wa Karen.

Huku akiwa amevalia barakoa nyeupe na mavazi na vyatu vya mazoezi, Bw Odinga aliandika hivi chini ya video hiyo: “Nafurahi kurejelea nyumbani.”

Katika video hiyo kiongozi huyo anasikika akizungumza na bintiye Winnie Odinga akisema “nahisi vizuri na nimefurahi kurejea nyumbani kufurahia mandhari.”

“Ni vizuri kwamba umerejea nyumbani baba, nyoosha magoti yako. Najitenga nawe kwani wewe ni kama mtu aliyepatikana na ugonjwa wa ukoma,” akasema Winnie.

Bw Odinga alifafanua kuwa japo amerejea nyumbani, bado atajitenga hadi wakati ambapo madaktari wake watamruhusu kutangamana na watu.

Wiki jana, kiongozi huyo wa ODM alilazwa katika Nairobi Hospital huku ikisemekana kuwa alikuwa akihisi uchovu.

Hii ni baada yake kurejea Nairobi baada ya kufanya ziara ya siku tano katika eneo la Pwani kuupigia debe Mswada wa Marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Baada ya siku mbili, daktari wake David Oluoch-Olunya, akafichua kuwa vipimo vimeonyesha kuwa alikuwa ameambukizwa Covid-19.

Hata hivyo, Olunya alitoa hakikisho kuwa Bw Odinga alikuwa katika hali nzuri akipokea matibabu.

“Kufuatia barua yangu ya Machi 10, 2021, tumethibitiasha kuwa Mheshimiwa Odinga amepatikana na ugonjwa wa Covid-19. Tunaendelea kufuatilia hali yake,” taarifa hiyo ikasema.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga alisema kwenye taarifa, pia alifanyiwa vipimo mbalimbali na mojawapo ya matokeo ambayo angependa kutangaza hadharani ni kwamba ameambukizwa corona.

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA