• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Zaha ndiye mchezaji wa kwanza wa EPL kususia utaratibu wa kupiga goti kabla ya mechi

Zaha ndiye mchezaji wa kwanza wa EPL kususia utaratibu wa kupiga goti kabla ya mechi

Na MASHIRIKA

FOWADI Wilfried Zaha wa Crystal Palace ndiye mwanasoka wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutopiga goti kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi kuanza.

Zaha alisalia akisimama tisti uwanjani wakati wenzake wote pamoja na wachezaji wa wapinzani wao West Bromwich Albion wakipiga goti katika juhudi za kukabiliana na ubaguzi wa rangi.

Kwa mujibu wa Zaha ambaye ni raia wa Ivory Coast, yeye ataendelea kufanya hivyo kwa sababu yapo mambo mengi zaidi yanayostahili kufanywa na vinara wa soka ili kukomesha uovu huo wa ubaguzi wa rangi zaidi ya kuhimiza wachezaji kupiga goti.

Mnamo Februari 2021, Zaha ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United, alisema kwamba hataendelea tena kufuata utaratibu huo wa kupiga goti kabla ya mechi uliokumbatiwa na vikosi vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita wa 2019-20.

Wachezaji wa EPL walianza kupiga goti kabla ya mechi ili kuunga mkono na kupiga jeki vuguvugu la ‘Black Lives Matter’ lililopata mashiko baada ya kuuawa kwa Mmarekani mweusi George Floyd nchini Amerika mnamo Mei 2020.

“Maamuzi yangu ya kutopiga goti kabla ya mwanzo wa mechi ni suala ambalo limefahamika kwa wiki kadhaa sasa,” akatanguliza Zaha.

“Hakuna maamuzi mazuri au mabaya kwa sababu nahisi kwamba kupiga goti ni jambo ambalo limekuwa la kawaida mno kiasi kwamba kwa sasa halina athari kubwa katika vita vya kukabiliana na ubaguzi wa rangi. Ajabu ni kwamba licha ya wanasoka kupiga goti, baadhi yetu bado tunabaguliwa kwa msingi wa rangi,” akaongeza.

Mechi dhidi ya West Brom ilikuwa ya kwanza kwa Zaha kupata fursa ya kudhihirisha msimamo wake baada ya kupona jeraha la paja lililomkosesha jumla ya michuano mitatu ya awali iliyosakatwa na Palace.

Nahodha wa Palace, Luka Milivojevic amesema anamuunga mkono Zaha kwa asilimia 100.

“Tunafanya hivyo (kupiga goti) ili tuwe mfano. Watoto wanapotuona na kutuuliza sababu ya hatua hiyo, wajue kwamba ubaguzi wa rangi ni kitu kibaya. Naheshimu sana hatua ya Zaha kwa sababu yeye amepania kukabiliana na uovu huo kwa njia nyingine tofauti kabisa,” akasema Milivojevic.

Kwa upande wake, kocha Roy Hodgson aliongeza: “Nitashangaa sana iwapo yeyote atafikiria kwamba Zaha hapigi goti tena kabla ya mechi kwa sababu hajali kabisa suala la ubaguzi wa rangi. Anafanya hivyo kwa sababu ni jambo linalomhusu sana. Ujumbe wake ni kwamba kinachofanywa kwa sasa hakina athari kubwa katika kukomesha uovu wenyewe.”

Zaha sasa anaungana na vikosi vya Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) – Derby County, Bournemouth na Brentford kutopiga goti tena kabla ya mechi.

Mwanzoni mwa msimu huu, Queens Park Rangers (QPR) pia waliacha kufanya hivyo baada ya mkurugenzi wao wa soka, Les Ferdinand kusema kwamba athari za kupiga goti ili kukabiliana na ubaguzi wa rangi “zimeyeyushwa”.

Hata hivyo, Richard Masters ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa EPL, amesema zoezi hilo litaendelea hadi mwisho wa msimu huu ila akakiri kwamba ipo haja kwa wanasoka wote wa EPL kuzungumziwa ili wapendekeze njia mwafaka na faafu zaidi ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Raila aondoka hospitalini, kuendelea kujitenga nyumbani

Quins, Blak Blad hatimaye wazoa ushindi Ligi Kuu ya Raga