• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Vijana wataka wapewe nafasi katika miradi ya ujenzi wa barabara nchini

Vijana wataka wapewe nafasi katika miradi ya ujenzi wa barabara nchini

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wanastahili kupewa nafasi katika miradi kadha ya ujenzi wa barabara zinazoendeshwa kupitia serikali chini ya Wizara ya Uchukuzi na Miundomsingi Dkt James Macharia.

Mwenyekiti wa vuguvugu la muungano wa vijana eneo la Mlima Kenya Bw Linford Mutembei, alisema serikali imekuwa ikiendeleza miradi kadha ya barabara kupitia Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA), ile ya barabara za mashinani KERRA na ile ya barabara za mijini KURA.

“Vijana wako katika mstari wa mbele kujiunga na miradi hiyo ili kujiendeleza kimaisha,” alisema Bw Mutembei.

Akizungumza na vijana mjini Ruiru kwa hamasisho kuhusu hali yao ya baadaye mnamo Jumamosi, alisema pindi tu miradi hiyo itakapokamilika biashara nyingi ndogo zitachipuka, viwanda na hata ujenzi wa majumba utashuhudiwa pakubwa.

“Kwa hivyo ni bora kujiweka tayari kuona ya kwamba unajiweka katika mstari wa mbele kujihusisha na mmojawapo wa miradi hiyo kwani ni njia moja ya kupata ajira,” alifafanua mwenyekiti huyo.

Alisema biashara zikipanuka mashinani bila shaka hali ya uchumi itaimarika kote nchini na vijana nao watanufaika pakubwa kuwa na ajira.

Alizidi kueleza kuwa ukarabati wa barabara katika kila sehemu utaimarisha maeneo ya mashinani huku wananchi wakipanua biashara zao kwa kiwango kikubwa.

Alisema serikali ya Uhuru Kenyatta, kupitia usimamizi wa mhandisi Peter Mundinia, tangu 2013, imekamilisha ujenzi wa barabara 49, huku 40 zikiwa bado zinaendelea kujengwa na zingine zinatarajia kuundwa zaidi.

Alitoa wito kwa serikali kupitia wahandisi wanaoendesha miradi hiyo kufanya jambo la busara kuona ya kwamba vijana wengi wanapewa nafasi kufanya kazi hizo ili kupunguza uhuni mashinani.

You can share this post!

Jeraha kumweka nje kiungo Doucoure wa Everton kwa wiki 10...

Familia zaanza kuhama kutoka Mto Ngong