Ruto amhepa Uhuru

Na MWANGI MUIRURI

MAKABILIANO ya kisiasa yaliyotarajiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja, huenda yasishuhudiwe.

Kiti hicho kiliachwa wazi kutokana na kifo cha mbunge Francis Munyua Waititu mnamo Februari 22 akiwa na miaka 62 baada ya kuugua kansa ya ubongo na uchaguzi mdogo umepangwa kufanyika Mei, 18.

Duru kutoka kwa wandani wa Rais na pia wa Naibu Rais katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) zinadokeza kwamba wawaniaji wa mrengo wa Naibu Rais walianza kuogopa vitisho kutoka kwa wafuasi sugu wa Rais ambao wanasimamia kampeni katika eneo hilo.

Mjane wa marehemu mbunge huyo Bi Susan Munyua anatarajiwa kuwania ubunge kwa tiketi ya Jubilee.

Kabla ya Marehemu Munyua kuwania ubunge 2013, alikuwa akifanya kazi kama meneja katika shamba la kahawa la familia ya Rais hivyo basi imani ya mjane kubakia katika mkondo wa siasa zitaungwa mkono na Rais Kenyatta.

Mwanasiasa George Koimburi na aliyekuwa meneja wa Hazina ya Ustawishaji Juja (NG-CDF) Bw Ken Gachuma pia wamekuwa wakisaka tiketi ya Jubilee.

Bi Eunice Wanjiru Willy alikuwa ametangaza waziwazi kuwa atawania kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Wadokezi wa Taifa Leo wasema uchunguzi uliofanywa na kitengo cha ujasusi ulionyesha kwamba Bi Munyua ana nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho. Inaaminika kwamba huenda hii ni sababu mojawapo iliyofanya UDA kuamua isijitose kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, kitengo hicho pia kilitoa ilani kwamba wapigakura wa Juja huwa na mtindo wa kukaidi serikali iliyo mamlakani.

Tayari, Bi Willy amehama chama cha UDA na kuingia kile cha The New Democrats (TND) chake mwanasiasa Thuo Mathenge, akisema kuwa alipata kidokezi kuwa chama cha Dkt Ruto hakitawania.

Kwa upande wake, Bw Gachuma ameamua kuwa mgombeaji wa kujitegemea.

“Jubilee ishaamua kuwa hakuna ushindani wa haki katika mchujo bali tunasakamwa tujiondoe na tumwachie mjane wa marehemu mbunge,” akalalamika Bw Gachuma.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Soy Bw Caleb Kositany ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, hakutakuwa na ushindani kati ya upande unaoegemea Rais Kenyatta na ule wa Dkt Ruto katika uchaguzi huo.

“Wale ambao wanatarajia kwamba kuna wakati wowote ambao Dkt Ruto atajitokeza waziwazi kukabiliana na Rais Kenyatta kuhusu suala lolote wanafaa waendelee kuota kwa kuwa hilo halitafanyika,” akasema Bw Kositany.

Huu pia ni msimamo uliotiliwa mkazo na mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua ambaye ni mmoja wa wanaompigia debe Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

“Sisi hatuna vita na Rais Kenyatta na kamwe hatutakubali kujiingiza katika mashindano naye. Tutazingatia maslahi mapana ya watu wa Juja na tuwaachie wafanye uamuzi utakaowafaa. Dkt Ruto ni Naibu wa Rais na Naibu kiongozi wa chama cha Jubilee na ikiwa mwaniaji wa Jubilee ndiye atakuwa kipenzi cha wengi katika eneo la Juja, sisi hatuna shida,” akasema.

Licha ya tetesi hizo, wadadisi wa kisiasa wamesema kuwa kile Dkt Ruto amefanya ni kubadili mbinu ya kisiasa kwa kutaka asionekane anamkabili Rais Kenyatta wazi wazi, japo huenda akafanya hivyo kichinichini.

Wakosoaji wake katika ukanda huo wamedai kwamba kuna uwezekano anafadhili mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria kumwakilisha katika kivumbi hicho kupitia chama chake.

“Tayari, Bw Koimburi amehama mrengo huo wa Jubilee na kujiunga na chama cha People Empowerment Party (PEP) chake Bw Kuria. Hii ina maana kuwa ushindani ukichambuliwa kwa msingi wa vyama vya kisiasa, kivumbi ni kati ya Rais na Bw Kuria,” akasema aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau.

Habari zinazohusiana na hii

KONDOO WA RUTO MATAANI