• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Shahidi katika kesi ya ufisadi apatikana ameuawa

Shahidi katika kesi ya ufisadi apatikana ameuawa

Na KITAVI MUTUA

AFISA wa cheo cha juu katika Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) Jennifer Itumbi Wambua, ambaye jana mwili wake ulipatikana katika msitu wa Ngong’, sasa imefichuka alitarajiwa kuwa shahidi mkuu katika kesi mbalimbali za ufisadi.

Wakili wa familia yake, Bw Daniel Maanzo, alisema marehemu alitarajiwa kutoa ushahidi katika mojawapo ya kesi za ufisadi hapo kesho.

“Alikuwa ni shahidi muhimu wa serikali katika kesi kadhaa zinazohusu ufisadi,” akasema Bw Maanzo.

Polisi waliuchukua mwili wa Bi Wambua na kuupeleka katika hifadhi ya maiti ya City, ambako ulitambuliwa na mumewe Joseph Komu pamoja na maafisa wa upelelezi.

Bi Wambua, ambaye alikuwa ametoweka Ijumaa iliyopita, ni mwanahabari mkongwe aliyewahi kuhudumu kwa miaka mingi kama Msimamizi Mkuu wa Shirika la Habari Nchini (KNA), Machakos, kabla ya kujiunga na NLC.

Hadi kufariki kwake, alikuwa ndiye Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano katika NLC.

Mama huyo wa watoto watatu alionekana mara ya mwisho Ijumaa asubuhi, wakati ambapo mumewe alimfikisha kazini kwa gari lao, kabla ya yeye kutoweka kiajabu saa chache baadaye.

Mkuu wa kitengo cha Upelelezi wa Jinai katika Kituo cha Polisi cha Kilimani, Nairobi, Bi Fatuma Hadi aliwaongoza maafisa wake na Bw Komu kutambua mwili wa Bi Wambua.

Bw Komu alisema kuwa baada ya kumfikisha mkewe katika afisi za tume hiyo ya ardhi Ijumaa asubuhi, alishangaa alipopata mkoba wake na simu yake ya mkono katika gari lao saa kadha baadaye akiwa katika gareji.

Bw Komu anafanyakazi katika makao makuu ya Wizara ya Kilimo, jumba la Kilimo, hatua chache kutoka jumba ambako Bi Wambua hufanya kazi.

Kulingana na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NLC Kabale Arero, Bi Wambua, mnamo Jumatatu wiki iliyopita, aliomba nafasi apumzike, akisema alikuwa akizongwa na mawazo.

“Alifika afisini mwangu Jumatatu Machi 8. Alinieleza jinsi alipata ajali wikiendi iliyotangulia na hata akanionyesha picha za gari lake lililoharibiwa,” akaeleza Bi Arero.

You can share this post!

Ruto amhepa Uhuru

Polisi waendelea kukamata wanaodai Magufuli anaugua