• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Ujenzi wa barabara wageuka kero kubwa kwa wakazi

Ujenzi wa barabara wageuka kero kubwa kwa wakazi

NA PAULINE ONGAJI

Kulingana na baadhi ya wakazi wa eneo hili vilevile wanaharakati wa kimazingira, baada ya shughuli hii kumalizika, kuliibuka masuala kadha ya kuhusu uharibifu wa mazingira.

Kigame Kisia, mwanaharakati wa kimazingira kutoka eneo hili anasema kwamba orodha ya masuala yanayoibua wasiwasi ni ndefu. “Mandhari ya sehemu hii imeathirika pakubwa. Pia, kuna tatizo la maji yaliyotuama ambayo ni mazingira mwafaka ya vimelea na magonjwa. Aidha, wakazi wanakumbwa na hatari ya kufa maji kwenye vidimbwi hivi,” aongeza.

Mzee Nerbert Ashiolo, 68, ambaye kipande chake cha ardhi kinapakana na sehemu hii, ni mmojawapo wa wakazi wanaolalamikia hali ilivyo.

“Kama mkazi yeyote anayeishi katika eneo hili, kila siku naishi na wasiwasi kwamba huenda wajukuu wangu wakafa maji kwenye vidimbwi hivi,” asema.

Lakini mbali na kuhofia usalama wao, anasema mafuriko pia yamekuwa jambo la kawaida kunaponyesha.

“Sehemu hii imekuwa ikikumbwa na mafuriko hasa kunaponyesha. Tumepoteza mimea na miti kutokana na mafuriko, jambo ambalo sikuwahi kushuhudia katika miaka ya awali,” aongeza.

Kama mmoja wa waathiriwa wakuu, anasema janga hili linafufua kumbukumbu ya waliyopitia wakati shughuli za ujenzi zilipokuwa zikiendelea.

“Mbali na kelele kutokana na mitambo hiyo, tulilazimika kuvumilia vumbi tele,” asema. Phillip Marigi, anayeishi mbali kidogo, anasema kwamba mafuriko ya kila mara hasa mvua inaponyesha, yamekuwa ya kawaida.

“Kila kunaponyesha, tunashindwa kuingia kijijini kwa kutumia njia kuu kwani mara nyingi hufurika,” aongeza. Kulingana na Marigi, mafuriko yalianza baada ya kampuni hiyo kuondoka.

“Mwanzoni, sehemu hii iligeuka na kuwa kama ziwa. Tokea wakati huo, tunaishi kwa hofu kwamba huenda siku moja tukasombwa na maji,” aongeza.

Huku baadhi ya wakazi na wanaharakati wa mazingira wakiendelea kupaza sauti zao kuhusiana na suala hili, kuna wale wanaosisitiza kwamba hakuna sheria za kimazingira zilizokiukwa katika shughuli hizi za ujenzi.

Mzee Nerbert Ashiolo, 68, mmoja wa wakazi wa eneo la Iribo, akilalamika kuhusu hali ilivyobadilika baada ya shughuli za uvunjaji mawe ya kokoto katika eneo la Iribo, Kaunti ya Nandi. Picha/ PAULINE ONGAJI

Kulingana na James Meli, Naibu Mkurugenzi wa masuala ya mazingira na maliasili katika Kaunti ya Nandi, sehemu hii ilitumika tu kwa uunganishaji pamoja wa mashine za ujenzi, na hivyo uwezekano kuwa shughuli za kampuni hii zingesababisha uharibifu, haupo.

“Kuhusu shimo lililo na kina kirefu, hatujui kina chake kwani hatuna mitambo ya kutambua urefu wake,” aongeza.

Hisia hizi zinaungwa mkono na Ali Mwanzei, Naibu Mkurugenzi wa shughuli za nje katika Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira (NEMA).

“Kulikuwa na mtambo wa kusaga mawe ya kokoto. Mtambo huu ulikuwa ukipokea malighafi kutoka Kaunti ya Vihiga, kumaanisha kuwa hakukuwa na shughuli za uchimbaji mawe hapo. Kwa hivyo suala la mandhari ya eneo hili kuharibiwa ni porojo tu,” asema Bw Mwanzei.

Aidha, anaongeza kwamba rekodi za afisi yao zinaonyesha kwamba hawakupokea malalamishi yoyote ya matatizo ya vumbi katika kipindi chote cha mradi huo.

Lakini hata ikiwa hakukuwa na uchimbaji wa mawe katika sehemu hii, ukweli ni kwamba hali sio ya kawaida hapa, angaa kutokana na vidimbwi hivi vya maji.

Vincent Mahiva, Mkurugenzi wa Nema katika Kaunti ya Nandi, asema kwamba tatizo la kipekee lilikuwa masalio ya kokoto.

“Katika utaratibu wa kampuni hii kukamilisha shughuli zake hapa, sehemu hii bado ilikuwa na maji, na hivyo tulikuwa tunasubiri yaishe ili tuondoe bidhaa hii,” asema.

Bw Mahiva anasema kwamba kampuni hiyo haipaswi kulaumiwa kwa hili, huku akisisitiza kwamba hakuna hali ya hatari. “Tulienda hapo kama kikosi kilichojumuisha maafisa kutoka Kaunti ya Nandi – ambayo ndio inayomiliki kipande hiki cha ardhi, Nema na idara ya mazingira ya kaunti, na kuthibitisha kwamba utaratibu ulifuatwa vilivyo,” aongeza.

Kuhusu maji yaliyotuama katika baadhi ya sehemu hizo, anasema kwamba, awali sehemu ya mwisho ya kipande hicho cha ardhi ilikuwa na maji, kumaanisha kwamba maji yaliyojikusanya hayakutokana na shughuli za kampuni husika.

“Tatizo kuu ni maji yaliyotuama ambayo hayawezi husishwa na shughuli za kampuni hiyo. Ni jambo la kawaida kwani tumeshuhudia visa vya ongezeko la maji katika maziwa mbalimbali nchini,” akaongeza Bw Mahiva.

Aidha anasisitiza kwamba, kampuni hiyo ilipoondoka, ilifanya kilichohitajika kuambatana na utaratibu wa kukamilisha shughuli za aina hii.

“Utaratibu ufaao ulifuatwa kuhakikisha kwamba sehemu hii ni salama. Aidha, kampuni hii ilijenga ua kabla ya kuipokeza sehemu hii kwa Kaunti ya Nandi, ambapo tuliridhika,” asisitiza.

Kulingana na Bw Mwanzei hakuna utaratibu uliokiukwa.

“Kilichosalia tu ni kokoto, bidhaa iliyotwaliwa kwa jamii. Mkandarasi aliambiwa ajenge kibao cha barabarani chenye maandishi “you are now crossing the equator” kwa minajili ya utalii. Serikali ya Kaunti ya Nandi inapanga kutumia sehemu hii kama eneo la kitalii,” anasema.

Kwa sasa wakazi wa Iribo wanachosalia nacho tu ni kumbukumbu ya sehemu hii ambayo awali ilikuwa kinamasi. Kwa upande mwingine, Nema yasisitiza kwamba kwa kiwango fulani, wakazi pia wanapaswa kulaumiwa.

“Kwanza, usalama unaanza nawe. Naambiwa kwamba kampuni hiyo iliweka ua katika sehemu hiyo, lakini ukaharibiwa na wakazi na vifaa kuibiwa,” aongeza Bw Mwanzei.

Hata hivyo, jitihada zetu za kutaka kupata maelezo zaidi kutoka kwa Covec-Kenya, kampuni husika kuhusu suala hili ziligonga mwamba.

You can share this post!

Polisi waendelea kukamata wanaodai Magufuli anaugua

Mhudumu wa afya afariki baada ya kuchanjwa Astra Zeneca