• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Mhudumu wa afya afariki baada ya kuchanjwa Astra Zeneca

Mhudumu wa afya afariki baada ya kuchanjwa Astra Zeneca

AFP Na SAMMY WAWERU

MHUDUMU mmoja wa afya Norway ameripotiwa kufariki kutokana na tatizo la ubongo baada ya kupewa chanjo ya AstraZeneca.

Idara ya afya nchini humo imetangaza, ila haijaeleza uhusiano wowote wa maafa hayo na chanjo ya AstraZeneca.

Kifo cha mhudumu huyo ni kisa cha pili kuripotiwa katika mataifa ya Bara Uropa, baada ya kusimamisha utopaji wa chanjo hiyo Alhamisi, juma lililopita.

Jumamosi, idara ya afya Norway ilisema wahudumu watatu wa afya nchini humo walilazwa hospitalini kwa sababu ya mgando wa damu mwilini, kufuja damu na upungufu wa chembechembe za damu.

Watatu hao wana umri chini ya miaka 50, ikisemekana walikuwa wamepata dozi ya kwanza ya chanjo hiyo iliyotengenezwa na kundi la watafiti wa dawa la Anglo-Swedish.

Mmoja wao aliyebainika kuwa mwanamke na aliyetajwa “kuwa katika hali nzuri kiafya”, aliaga dunia Jumapili kwa kile idara ya afya Norway ilisema ni tatizo la ubongo.

Duru zinaarifu mhudumu huyo alilazwa hospitalini Alhamisi, wiki moja baada ya kupata chanjo ya AstraZeneca.

“Hatuwezi tukathibitisha wala kupinga maafa yake yanahusishwa na chanjo ya AstraZeneca,” Steinar Madsen, afisa kutoka kitengo cha taasisi ya dawa Norway akaambia wanahabari.

Hali ya wahudumu wawili waliosalia inaendelea kuimarika. Mhudumu mwingine anayesemekana kuwa katika miaka ya 30 alifariki Ijumaa Norway, siku 10 baada ya kupata chanjo hiyo.

Visa vya maafa vimeripotiwa Bara Uropa, hasa Austria na Denmark, baada ya kuchanjwa.

Taasisi inayoshughulikia masuala ya dawa Uropa inaendelea kufanya uchunguzi wa visa hivyo, kubaini iwapo vinahusishwa na chanjo ya AstraZeneca.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Ijumaa, wiki iliyopita, lilisema “hatujaona sababu ya kutoitumia”, huku kampuni ilyotengeneza chanjo hiyo ikisisitiza ni salama.

Kulingana na Idara ya Afya Norway, karibu watu 130, 000 walikuwa wamepata chanjo hiyo kabla kusimamishwa.

Nchi ambazo zimesimamisha usambazaji wa AstraZeneca kufuatia sababu sawa na za Norway ni pamoja na Denmark, Iceland, Bulgaria, Ireland, Netherlands, France, Italy na Germany.

Denmark ilikuwa nchi ya kwanza kusimamisha utoaji wa chanjo hiyo Alhamisi, juma lililopita, baada ya kuandikisha kisa cha kwanza cha maafa kilichohusishwa na AstraZeneca.

Aidha, kisa hicho kiliripotiwa Jumatatu juma hilo, mwathiriwa akitambuliwa kuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 60.

Ripoti ya matibabu ilionyesha aliganda damu mwilini, kupungua kwa chembechembe za damu na pia tatizo la ubongo, baada ya kuchanjwa.

Idara ya afya Denmark imewataka waliopata chanjo hiyo chini ya majuma mawili yaliyopita kutilia maanani dalili wanazoshuhudia kama vile majeraha yasiyo ya kawaida, kufuja damu mwilini, maumivu ya kichwa na tumbo.

Karibu watu 150, 000 Denmark wamepata chanjo ya AstraZeneca dozi ya kwanza, na 583 dozi ya pili.

Afrika Kusini pia ilikuwa imesimamisha utoaji wa chanjo hiyo kwa muda, baada ya kuonekana kutokabili aina mpya ya virusi vya corona.

Licha ya Bara Uropa kusimamisha chanjo ya AstraZeneca, Kenya inaendelea kuisambaza.

Kwenye hotuba yake kwa taifa Ijumaa, Rais Uhuru Kenyatta aliondolea Wakenya hofu ya chanjo hiyo, akiwahakikishia kwamba serikali iko macho kuhusu hali zozote ambazo huenda zikatokea.

“Hakuna tatizo ambalo limeibuka nchini kufikia sasa. Wahudumu wetu wa afya wako macho kuhakikisha watashughulikia suala lolote ambalo huenda likatokea miongoni mwa wale ambao tayari wamepewa,” akasema Rais.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth alikuwa Mkenya wa kwanza na afisa wa kwanza wa afya kupata chanjo hiyo.

You can share this post!

Ujenzi wa barabara wageuka kero kubwa kwa wakazi

Uchunguzi waanzishwa kufuatia kifo cha mfanyabiashara Thika