• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Vitambulisho vya kitaifa kufutiliwa mbali, Huduma Namba kutumika

Vitambulisho vya kitaifa kufutiliwa mbali, Huduma Namba kutumika

Na SAMMY WAWERU

Serikali imesema itafutilia mbali vitambulisho vya kitaifa mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.

Msemaji wa serikali, Kanali Cyrus Oguna amesema Jumanne kwamba kadi ya Huduma Namba ndiyo itatumika kama utambulisho wa kitaifa.

Bw Oguna alisema tayari Wakenya milioni 4.5 wametumiwa ujumbe wa kuchukua kadi hiyo.

“Kadi ya Huduma Namba iko tayari. Tunaomba wote waliojiandikisha, kuchagua kituo au eneo ambalo itatumwa ili waichukue,” akasema.

Kanali Oguna pia alisema asilimia 50 ya waliotumiwa ujumbe ndio wamechukua kadi zao kufikia sasa.

“Kitambulisho cha kitaifa kitafutiliwa mbali pindi tutakapochapisho tangazo hilo katika Gazeti Rasmi la Serikali,” Bw Oguna akasema, akiashiria uwezekano wa hatua hiyo kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa ujao.

Zoezi la Wakenya na raia wa kigeni walioko nchini kujiandikisha kupata kadi ya Huduma Namba lilifanyika kati ya Aprili 25, 2019 na Mei 29, 2019.

Mwaka uliopita, 2020, serikali ilikuwa imetangaza itazindua awamu ya pili ya usajili, kwa wale ambao hawakuwa wamejiandikisha.

Takwimu za serikali zinaonyesha watu wapatao milioni 31 ndio walijiandikisha kupata Huduma Namba.

You can share this post!

Kenya ilipoteza Sh560 billioni kutokana na corona 2020 –...

CECIL ODONGO: Kadhi Mkuu mpya sasa atoke eneo jingine la...