Hofu wanaofariki baada ya kupata chanjo wakiongezeka

Na AFP

IDADI ya watu wanaofariki baada ya kupokea chanjo ya kuepusha virusi vya corona ya AstraZeneca, imezidi kuongezeka.

Mhudumu wa afya nchini Norway alifariki kutokana na kuvuja damu kwenye ubongo baada ya kupokea chanjo hiyo dhidi ya Covid-19.

Hakuna uhusiano wa moja kwa moja na chanjo hiyo uliothibitishwa, wizara ya afya nchini humo ilisema Jumatatu.

Kisa hiki cha mtu kufariki ni cha pili kutokea hivi majuzi katika taifa hilo lililokuwa limesitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kama mikakati ya kujikinga Alhamisi iliyopita.

Mnamo Jumamosi, serikali ya Norway ilisema wahudumu watatu wa afya walilazwa hospitalini wakiwa na matuta ya damu, kuvuja damu na viwango vya chini kupindukia vya chembechembe za damu.

Wote walikuwa wenye umri chini ya miaka 50, na wote walikuwa wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo hiyo iliyoundwa na kampuni ya dawa kutoka Uswizi.

Mmoja miongoni mwa watatu hao, aliyetajwa kama mwanamke “mzima kiafya” alifariki Jumapili baada ya kuvuja damu kwenye ubongo, wizara ya afya ilisema.

Alilazwa hospitalini mnamo Alhamisi, karibu wiki moja baada ya kupokea chanjo hiyo. “Hatuwezi tukathibitisha au kukanusha kwamba visa hivyo vinahusiana na chanjo,” afisa mmoja kutoka Shirika la Dawa Norway, Steinar Madsen, alieleza wanahabari.

Hali ya maafisa hao wengine wawili iliripotiwa kuwa shwari. Mhudumu mwingine wa afya katika miaka ya 30 alifariki mnamo Ijumaa nchini Norway, siku 10 baada ya kupokea chanjo hiyo.

Vifo vingine vimeripotiwa vilevile barani Uropa hususan Austria na Denmark.

Eneo la Kaskazini la Piedmont, nchini Italy, mnamo Jumapili lilisitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca baada ya kifo cha mwalimu aliyekuwa ameipokea siku moja iliyotangulia, wizara ya afya nchini humo ilisema.

Mwanamke huyo, ambaye umri wake haujafichuliwa, alifariki Jumapili eneo la Biella, mji wa kaskazini wa Turin.

Shirika la Dawa Uropa kwa sasa linachunguza vifo hivyo kuona iwapo vinahusiana na chanjo hiyo.

Mnamo Ijumaa, Shirika la Afya Duniani lilisema hakuna “ishara ya kukosa kutumia,” huku kampuni yenyewe iliyounda chanjo hiyo ikisisitiza kuwa ni salama.

Kulingana na mamlaka ya tiba Norway, watu wapatao 130,000 walikuwa wamepokea chanjo hiyo kabla ya kusitishwa.

Miongoni mwa mataifa mengine ambayo pia yamesitisha chanjo hiyo kwa sababu sawa na hizo ni Denmark, Iceland, Bulgaria, Ireland, Uholanzi, Ufaransa, Italia na Ujerumani.

Habari zinazohusiana na hii