• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
MAFUTA: Wakenya wakimbilia Tanzania

MAFUTA: Wakenya wakimbilia Tanzania

IAN BYRON NA HILLARY KIMUYU

MAMIA ya Wakenya wanavuka mpaka hadi nchi jirani za Tanzania na Uganda kununua mafuta kwa bei nafuu.Hii ni baada ya serikali ya Kenya kupandisha bei ya bidhaa hiyo nchini kwa kiasi kikubwa, hali ambayo imelemewa mamilioni ya Wakenya.

Tangu Jumatatu, wakazi wa kaunti za Migori, Kisii, Homa Bay na Busia wamekuwa wakivuka mpaka wa Kenya na Tanzania pamoja na Uganda, ili kununua mafuta ya bei nafuu katika nchi hizo majirani.Bei ya mafuta ni nafuu nchini Uganda licha ya kuwa taifa hilo hutegemea Kenya kupokea mafuta yake kutoka nchi za nje.

Mnamo Jumapili, Mamlaka ya Kudhibiti Biashara za Mafuta na Kawi (EPRA) ilitangaza ongezeko la bei za mafuta kwa mwezi wa nne mfululizo.

Katika Kaunti ya Migori, mafuta ya petroli, dizeli na mafuta taa yanauzwa kwa Sh130.11, Sh120.26 na Sh99.07 mtawalia kwa kila lita, ikilinganishwa na nchi ya Tanzania ambapo petroli, dizeli na mafuta taa zinauzwa Sh94, Sh90 na Sh88 mtawalia.

“Heri ninunue mafuta kwa bei nafuu katika nchi jirani ambako petroli lita moja ni Sh94 ikilinganishwa na Kenya tunakouziwa petroli lita moja Sh130. Tutaendelea kununua mafuta huko na kujenga uchumi wa nchi majirani kwa kuwa serikali yetu ya Kenya imekataa kusikiza kilio chetu,” Bw Peter Onyonka aliambia Taifa Leo.

Hali hiyo imeshuhudiwa katika sehemu za Isebania, ambapo waendeshaji bodaboda tangu Jumatatu wamekuwa wakivuka mpaka eneo la Sirare wakiwa wamebeba mitungi ya mafuta kwa kuwauzia wenzao upande wa Kenya kwa bei nafuu.

Waendeshaji bodaboda hao walisema wanaumia sana kutokana na ongezeko la bei za mafuta, kwani wateja hawakubali kulipa nauli za juu.Kutokana na malalamishi ya wanachi kuhusu ongezeko la bei za mafuta, EPRA ilijitetea ikisema kuwa maamuzi ya bei za mafuta hulingana na hali ilivyo kimataifa.

EPRA pia ilijitetea ikisema kuwa bei ya kuagiza petroli, dizeli na mafuta taa kimataifa ilipanda kutoka mwezi uliopita.Kufuatia malalamishi ya wananchi, serikali kupitia kwa msemaji wake, Cyrus Oguna imewakashifu Wakenya ikiwataka wakome kulalamika kwa kutozwa ushuru wa juu, ‘kwani inahitaji pesa nyingi’.

Katika kikao cha wanahabari Nairobi, Bw Oguna alisisitiza kuwa Wakenya wanastahili kutozwa ushuru wa juu, na hivyo serikali haijakosea kwa kuongeza bei ya mafuta.

“Serikali ina jukumu la kupeana huduma. Kuna polisi, wanajeshi na watumishi wa umma kama sisi ambao lazima tulipwe. Kuna barabara, hospitali na shule ambazo lazima ziwepo,” akasema

.“Kiwango cha ushuru ambacho watu hulipa Ulaya ni mkubwa mno kuliko ilivyo hapa. Kwa hivyo tunalia wakati hatupaswi kulia. Tunafaa kusimama kidete kusaidia serikali. Tusiwe watu wa kulialia kila mara,” akasema.

Matamshi ya Bw Oguna yamezua hasira kutoka kwa Wakenya ambao wanalemewa na ugumu wa maisha kutoana na kuzorota kwa uchumi, ufisadi na huduma duni zinazotolewa na serikali kwao.

Wakenya waliomsuta Bw Oguna katika mitandao ya kijamii walitaka kujua ikiwa serikali ya Kenya hutoa huduma bora kwa wananchi sawa na jinsi ilivyo Ulaya, kiwango cha ufisadi wa kupora mali ya umma katika mataifa hayo, na adhabu inayotolewa kwa watumishi wa umma au mwananchi yeyote anayeshtakiwa kwa ufisadi.

You can share this post!

Rais wa Tanzania John Magufuli afariki

Maeneobunge 70 zaidi ni haramu – Chebukati