• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:15 AM
WANDERI KAMAU: Tujuzwe sababu za bei ya mafuta kupanda kila siku

WANDERI KAMAU: Tujuzwe sababu za bei ya mafuta kupanda kila siku

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya masuala ambayo huibua ghadhabu miongoni mwa wananchi ni pale serikali inawatwika mizigo ya kimaisha bila kujali.

Katika hali hiyo, wananchi huungana na kuwakabili watawala waliopo bila kujali athari za kisiasa, kiuchumi na kijamii.Mwenendo huo ndio ulizua ghadhabu miongoni mwa wenyeji wa Ufaransa mnamo 1789, ambapo waliukabili utawala wa kifalme kwa kuongeza bei ya mkate ovyo bila kuwashauri wananchi.

Wenyeji waliutaka utawala huo kuwaeleza sababu kuu ya kuongeza bei hizo, ilhali mkate ndio ulikuwa chakula chao cha msingi.Ghadhabu zilizoibuka ndizo zilikuwa msingi wa kusambaratika kwa utawala huo.

Nchini Sudan, mwelekeo uo huo ndio ulisababisha aliyekuwa rais wa taifa hilo, Omar el Bashir, kungatuliwa mamlakani mnamo 2018.Licha ya kufahamu mkate ni miongoni mwa chakula kinachotegemewa sana na raia wa taifa hilo, utawala wa Bashir ulikosa kuchukua hatua zifaazo kudhibiti ongezeko la bei yake.

Maelfu ya raia waliandamama kuikashifu vikali serikali yake, wakiitaja kuwa ya kibepari na isiyojali maslahi yao.Matokeo ya ghadhabu hizo yalikuwa kuondolewa mamlakani kwa Bashir na washirika wake wote.

Vivyo hivyo, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inapaswa kutahadhari matokeo ya kuongeza ovyo bei za mafuta bila kuwashirikisha wananchi ama taasisi zifaazo.

Tangu Januari, bei za mafuta nchini zimekuwa zikiongezeka kwa kasi katika hali tatanishi.Ni hali ambayo imewafanya Wakenya wengi kulalamikia ongezeko la gharama ya maisha bila kupata jibu kutoka kwa serikali.

Badala yake, viongozi wote husika wamenyamaza. Hakuna hata mmoja aliyejitokeza kutafuta ufafanuzi kamili kutoka kwa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) kuhusu chanzo cha ongezeko la bei hizo.Kimsingi, kinachozua maswali ni ripoti kuwa bei za mafuta nchini ziko juu ikilinganishwa na mataifa jirani kama Uganda, Tanzania na Rwanda.

Kinaya ni kuwa, nchi kama Uganda na Rwanda huwa zinatumia Bandari ya Mombasa kusafirishia mafuta yao. Je, ni vipi tena mafuta hayo ni ghali Kenya ikilinganishwa na nchi hizo?

Kuna njama ya siri inayoendeshwa na watu wenye ushawishi serikalini kuwapunja Wakenya? Ni nani atatoa ufafanuzi kamili kuhusu mwelekeo huu?Bila shaka, hili ni suala linalohitaji ufafanuzi kamili.

Kufikia sasa, petroli imeongezeka kwa karibu Sh15 kwa miezi miwili pekee. Hali iyo hiyo ndiyo inayowakumba wale wanaotumia dizeli na mafuta taa. Hata ikiwa dunia nzima inakumbwa na changamoto za kiuchumi, ongezeko hilo si la kawaida!

Swali jingine lililopo ni kuwa karibu miaka miwili iliyopita, Wakenya walijawa na matumaini baada ya Rais Kenyatta kuzindua usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Kaunti ya Turkana hadi nchi za nje ili kusafishwa. Je, uzinduzi huo ulikuwa kifungamacho? Mbona serikali inawachezea Wakenya shere?

Katika wakati huu ambapo kila mmoja analia kuhusu ugumu wa maisha kutokana na athari za janga la virusi vya corona, serikali haipaswi kuwasaliti wananchi kwa sera kama hizo. [email protected]

You can share this post!

Maeneobunge 70 zaidi ni haramu – Chebukati

KINYUA BIN KING’ORI: Tusipuuze athari za corona hata...