• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Upinzani TZ wataka Mama Samia Suluhu kuapishwa kuwa Rais mara moja

Upinzani TZ wataka Mama Samia Suluhu kuapishwa kuwa Rais mara moja

Na MARY WANGARI

VIONGOZI wa upinzani nchini Tanzania wametoa wito kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa mara moja kama Rais huku chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM) kikitangaza siku 21 za kumwomboleza marehemu Rais John Pombe Magufuli.

Wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa Chama cha Alliance for Change and Transparency Wazalendo, ACTWazalendo, Zitto MwamiRuyagwa Kabwe, wamemtaka Naibu Rais Suluhu kuapishwa mara moja kama rais.

Wamehoji kuwa hatua hiyo itazuia hali ya kiti cha rais kubaki tupu na vilevile kuepusha wingu la taharuki kutanda nchini humo.

“Naibu Rais wa Tanzania Suluhu Samia ni sharti aapishwe mara moja kama rais kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli,”

“Hii ni kwa sababu katiba hairuhusu kuwepo “utupu” kwenye kiti cha urais,” kiongiozi huyo wa upinzani alieleza vyombo vya habari nchini humo mnamo Alhamisi, Machi 18, 2021.

Serikali bado haijasema lolote kuhusu mipango ya kumrithi marehemu Magufuli ambaye ni rais wa kwanza kufariki akiwa mamlakani katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

“Katika kipindi hiki kigumu, tunamtazama rais anayeingia kutua uongozi na umoja tunaohitaji. Tunamtakia baraka, ujasiri na subra,” aliandika Kabwe kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kauli yake imejiri siku moja tu baada ya Naibu Rais Suluhu kutangaza kifo cha Magufuli lakini hakusema lolote kuhusu ni lini ataapishwa kama rais.

Kulingana na Katiba ya Tanzania, Makamu wa Rais ndiye anayepaswa kuchukua usukani endapo rais anayetawala atafariki akiwa angali afisini.

Endapo ataapishwa kama rais, Suluhu mwenye umri wa miaka 61, ataingia kwenye vitabu vya historia kama rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na barani Afrika Mashariki kwa jumla.

Suluhu alitangaza kuhusu kifo cha Rais Magufuli pamoja na siku 14 za kumwomboleza mnamo Jumatano, Machi 17, 2021.

Kulingana na katiba ya Tanzania muda wa kumwomboleza kiongozi wa taifa baada ya kuaga dunia ni siku 21.

Kipindi cha maombolezi kilichotangazwa na CCM Alhamisi, Machi 18, 2021, ni siku saba zaidi ya muda wa maombolezi uliotangazwa na Suluhu, alipopasua mbarika kuhusu kifo cha Magufuli.

Wadadisi wametaja hatua hiyo ya Suluhu kutangaza upesi kifo cha Magufuli kama mikakati kabambe iliyomwezesha kuwafumania washindani wake waliokuwa wakijishughulisha kupanga namna ya kumrithi marehemu rais wa Tanzania.

You can share this post!

SAMIA SULUHU: Rais mtarajiwa wa Tanzania

Magufuli ameangamizwa na corona, Tundu Lissu adai