Magufuli ameangamizwa na corona, Tundu Lissu adai

Na SAMMY WAWERU

Kiongozi wa upinzani Tanzania Bw Tundu Lissu amedai Alhamisi Rais wa nchi hiyo, Dkt John Pombe alifariki kutokana na virusi vya corona.

Bw Lissu ametaja kifo cha Dkt Magufuli kama “shairi la haki”, baada ya Rais huyo kupuuza na kukana kuwepo kwa Covid-19 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamu wa Rais wa taifa hilo, Bi Samia Suluhu Hassan akitangaza rasmi kifo cha Rais Magufuli Jumatano, alisema kiongozi huyo ambaye hajaonekana machoni pa umma kwa muda wa wiki kadhaa, alifariki kutokana na tatizo la moyo baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwenye hotuba yake, Bi Samia alisema Rais Magufuli aliaga wakati akiendelea kupata matibabu katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kulingana na Bw Lissu na ambaye mwaka uliopita, Oktoba 2020 alitoana kijasho na Rais huyo katika uchaguzi mkuu amesema Dkt Magufuli, 61, aliangamizwa na virusi vya corona.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema serikali ya Tanzania inaendelea “kusakata na kueneza uongo hata wakati huu amefariki”.

“Magufuli alifariki kutokana na corona,” akasema Bw Lissu ambaye yuko mafichoni Ubelgiji, kupitia mahojiano na runinga ya KTN News, huku akifichua wajuzi wake. Madai hayo hata hivyo hayajathibitishwa.

Lissu alienda mafichoni Ubelgiji kufuatia kuendelea kuandamwa na kuhangaishwa na serikali ya Rais Magufuli, baada ya kukosoa alivyochaguliwa katika uchaguzi wa 2020 na aliotaja ulijawa utapeli na wizi wa kura.

Kutoonekana kwa magufuli hadharani majuma kadhaa kulizua hisia mseto miongoni mwa umma nchini humo na pia mataifa jirani, tetesi kuhusu hali yake ya afya zikisambaa mitandaoni na pia kuangaziwa na vyombo vya habari.

Aidha, wapinzani wake walidai aliugua corona na ndio sababu serikali ilisalia kimya. Serikali ya Tanzania hata hivyo ilikana madai hayo.

Rais Magufuli ni kati ya viongozi waliopuuzilia mbali na kupinga kuwepo kwa Covid-19 Tanzania, akihimiza raia wa nchi yake kukumbatia dawa asilimia na kutovalia barakoa.

Alitilia mkazo maombi, akisema Mungu ameepushia Tanzania janga la corona.

Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku kutangazwa kwa takwimu za maambukizi ya Homa ya corona Aprili 2020 wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa imeandikisha visa 509 na wagonjwa 16 kuangamia.

Bw Lissu amesema ni “shairi la haki” Dkt Magufuli kuangamizwa na ugonjwa ambao alipuuza kuwepo.

“Rais Magufuli hakuwa akivalia maski. Alidunisha walioivalia. Hakuamini chanjo, hakuamini Sayansi,” akasema kiongozi huyo wa upinzani na ambaye 2017 alipigwa risasi mara kadhaa, katika kile alitaja kama njama ya kisiasa kumuondoa uhai.

“Aliweka imani yake kwa waponyaji waliokuwa na imani potovu, alitegemea dawa asilia na matibabu bandia. Yaliyofanyika yamefanyika. Corona imemuangusha,” Bw Lissu akaelezea kwenye mahojiano hayo.

Makamu wa Rais, Bi Samia Suluhu Hassan ametangaza kutenga siku 14 taifa la Tanzania kuomboleza Dkt Magufuli.

Habari zinazohusiana na hii