• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Magufuli ‘alitabiri’ kifo chake Februari

Magufuli ‘alitabiri’ kifo chake Februari

Na BENSON MATHEKA

RAIS wa Tanzania aliyeaga dunia, John Joseph Pombe Magufuli, ambaye kifo chake kilitangazwa Jumatano, alikuwa ametabiri kwamba angeenda jongomeo mwezi mmoja uliopita.

“Kufa tutakufa tu! Unaweza ukafa kwa malaria, ukafa kwa kansa, ukafa kwa magonjwa mengine, kwa sababu kufa kupo!” akasema Rais Magufuli mnamo Februari 19, 2021 kwenye mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma katika serikali yake, John William Kijazi.

Pia aliwataka raia wa Tanzania kutotishwa na maradhi ya Covid-19, ambayo yalimuua katibu huyo aliyekuwa mwandani wake wa karibu, akisema kwamba hata yeye alikuwa njiani kuelekea kaburini.

“Mungu ambariki sana marehemu John William Kijazi, najua na sisi tuko njiani tunakuja,” Magufuli aliambia waombolezaji.Kwenye hotuba yake, Rais Magufuli aliwataka raia wa Tanzania wasiogope kifo mbali wamtumaini na kumuomba Mungu kwa sababu kifo ni lazima kwa kila mtu.

Wiki moja baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli hakuonekana tena hadharani, hali iliyozua uvumi kwamba alikuwa katika hali mahututi akiugua Covid-19.Utawala wake ulipinga vikali madai hayo ukisema alikuwa katika hali shwari akiendelea na kazi zake kimya kimya.

Serikali hiyo ilivunja kimya hicho mnamo Jumatano usiku ilipotangaza kwenye televisheni ya taifa (TBC) kifo chake kutokana na kile Makamu wa Rais Samia Suluhu alitaja kuwa matatizo ya moyo.

Mhubiri alibashiri rais angeaga

Mnamo 2016, aliyekuwa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini na pia mhubiri, Godbless Lema, alitabiri kuwa Rais Magufuli ‘angekufa iwapo angeendelea na utawala wake wa mabavu.’

Kauli hiyo ilimfanya kuandamwa na maafisa wa polisi.’Mungu amenionyesha kwamba Rais Magufuli asipojirekebisha atakufa. Akiendelea kufikiri yeye ni Mungu na kuwa kila kitu kiko chini yake; akiendelea kucheza na maisha ya watu kwa sababu ya nguvu za dola, hatafikisha mwaka wa 2020,’ akasema Bw Lema, ambaye sasa yuko uhamishoni nchini Canada alikopata hifadhi kutokana na kuhangaishwa na utawala wa Tanzania.

Kiongozi mwingine wa upinzani wa Tanzania anayeishi uhamishoni nchini Ubelgiji, Tundu Lissu alikuwa wa kwanza kudai kwamba Rais Magufuli alikuwa amelazwa katika Nairobi Hospital jijini Nairobi baada ya hali yake ya afya kudorora akitibiwa Tanzania.

Kutoweka

“Rais Magufuli hakwenda kanisani Jumapili iliyopita na leo pia hajaenda. Hakuhudhuria mkutano wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wiki iliyopita na hajaonekana hadharani kwa zaidi ya wiki,’ Bw Lissu aliandika kwenye Twitter mnamo Machi 7.

Serikali ilipuuza madai yake na kuonya raia na vyombo vya habari dhidi ya kutangaza ama kuandika uvumi, na watu kadhaa walikamatwa.

Licha ya rais huyo kutoonekana hadharani kwa zaidi ya siku 10, maafisa wa serikali wakiongozwa na Bi Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mabalozi walisisitiza kuwa Magufuli alikuwa buheri wa afya na alikuwa akichapa kazi kama kawaida.Bw Lissu alisisitiza kuwa Rais Magufuli alikuwa amefariki na jeshi lilikuwa ikipanga utaratibu wa kutangaza rasmi kifo chake.

Magufuli aliyekuwa akihudumu muhula wa pili kama rais wa tano wa Tanzania alifariki akiwa na umri wa miaka 61.Alisomea katika shule na vyuo vikuu nchini Tanzania hadi akahitimu uzamili.

Alijiunga na siasa mwaka wa 1992 alipochaguliwa mbunge wa eneobunge la Chato.Kabla ya kuchaguliwa rais mara ya kwanza mnamo 2015, alikuwa amehudumu kama waziri wa ujenzi na barabara katika serikali ya Rais Benjamin Mkapa na waziri wa ardhi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

You can share this post!

Tundu Lissu asema atarejea Tanzania iwapo ataruhusiwa...

Magufuli hakuwa na wakati wa kuwabembeleza Wakenya