Magufuli aliiga Trump kupuuza corona

BENSON MATHEKA Na WINNIE A ONYANDO

VIRUSI vya corona vilipotangazwa kuwa janga la kimataifa mnamo Machi 2020, Rais John Pombe Magufuli aliyefariki jana, alikuwa miongoni mwa viongozi wa mataifa kadhaa, akiwemo Donald Trump wa Amerika waliopuuza hatari yake.

Wakati nchi nyingi ulimwenguni zilikuwa zikichukua hatua za kuzuia kusambaa wa virusi hivyo, Bw Magufuli aliambia Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Alitaja virusi hivyo kama homa ya kawaida na kwamba, hatari yake ilikuwa imeongezwa chumvi na mataifa ya kigeni.“Sitafunga kama nchi nyingine, endeeleni na shughuli zenu za kawaida, tieni bidii kazini tukuze chakula kwa wingi mashambani tuwauzie wale waliofunga nchi yao.

Wakija kununua chakula, wauzieni kwa bei ghali, wafinyeni kabisa,” alisema Bw Magufuli.Alikejeli nchi jirani kama Kenya na Uganda kwa kutangaza kafyu, kufunga shule, sehemu za ibada na michezo na kuwataka raia wa nchi yake kuomba Mungu na kuvalia barakoa.

Hadi kifo chake hakuwa amevalia barakoa hata siku moja. Mnamo Machi 16, aliagiza Wizara ya Afya kutotangaza idadi ya visa vya maambukizi ya corona wakati nchi hiyo ilikuwa imeripoti visa 509 na vifo 29 kinyume na kanuni za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Wakati huo, alisema serikali yake ilikuwa imeangamiza corona kupitia maombi na kutumia mbinu za kiasili za kutibu homa.“Corona imeangamizwa Tanzania na tunashukuru Mungu,” aliwaambia waumini katika kanisa Katoliki jijini Dodoma.

Hadi kifo chake Jumatano, Tanzania ilikuwa nchi ya pekee ulimwenguni ambayo haitangazi idadi ya maambukizi ya corona hatua ambayo ilitia wasiwasi wataalamu wa WHO.

Magufuli alidharau kanuni za WHO za kupima raia virusi vya corona akisema uchunguzi wake uligundua vipimo havingeaminika.

“Tulipima matunda na mbuzi na matokeo yakawa zina virusi vya corona,” alisema wakati huo. Mwezi jana, serikali ya Tanzania ilipuuza onyo la ubalozi wa Amerika nchini humo uliosema kwamba, hospitali jijini Dar es Salaam zilikuwa zimelemewa na wagonjwa wa corona na kwamba kulikuwa na hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo jijini humo.

Alikuwa msitari wa mbele kuwashauri raia kutovalia barakoa, kutodumisha umbali na kuwataka wahudhurie ibada katika makanisa na misikiti akisisitiza kuwa maombi yataangamiza maradhi hayo.

Wakati nchi nyingi zilikuwa zikikabilia na wimbi la pili la maambukizi, Magufuli aliwataka Watanzania kuomba kwa siku kadhaa.“Ninataka kushukuru Watanzania wa imani zote. Tumekuwa tukiomba na kufunga ili Mungu atuokoe kutoka janga hili ambalo limeathiri nchi yetu na ulimwengu. Lakini Mungu amejibu maombi yetu,” alisema.

“Ninaamini, ni niko na hakika Watanzania wengi wanaamini kwamba ugonjwa wa corona umeangamizwa na Mungu,” alisema.Hii ilikuwa licha ya viongozi wa makanisa na maafisa wakuu wa serikali yake kuuawa na ugonjwa huo.Wakati mataifa ulimwenguni yalikuwa yakishangilia na kuchangamkia upatikakanaji wa chanjo ya corona, Magufuli aliipuuza na kukataa katika nchi yake.

“Tunafaa kuwa waangalifu kwa kuwa baadhi ya misaada ya kupigana na corona inaweza kutumiwa kusambaza virusi hivyo.Alishangaa jinsi wataalamu wa mataifa ya Ulaya wanaweza kupata chanjo ya corona baada ya mwaka mmoja ilhali hawajapata chanjo ya Ukimwi na Malaria.

“Wizara wa Afya haina mpango yoyote wa kupokea chanjo kutoka nchi zingine.Tumieni mchanganyiko wa tangawizi, limau na kitungu saumu ili kudhibiti ugonjwa wa corona,” alisema kauli iliyosisitizwa na maafisa wa afya.

Mbali na Trump, viongozi wengine waliopuuza corona ni Jair Bolsonaro wa Brazil ambaye baadaye aliambukizwa virusi hivyo na aliyekuwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.

Habari zinazohusiana na hii