• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Samia Suluhu kuchukua usukani Tanzania kwa kipindi kilichosalia

Samia Suluhu kuchukua usukani Tanzania kwa kipindi kilichosalia

NA LEONARD ONYANGO 

NAIBU Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atakuwa rais wa sita kutawala Tanzania, na rais wa kwanza mwanamke nchini humo na Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli.

Kulingana na Katiba ya Tanzania, Naibu Rais ndiye anayechukua usukani kama rais na anatazamiwa kuliongoza taifa hilo kwa kipindi kilichosalia cha miaka minne.

Bi Suluhu aliye na umri wa miaka 61,alizaliwa katika Kisiwa cha Zanzibar mnamo Januari, 27, 1960, ambapo alikamilisha masomo yake ya sekondari mnamo 1977.Mnamo 1978, alifunga ndoa na Bw Hafidh Ameir, ambaye ni afisa mstaafu wa kilimo na pamoja wamejaaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na msichana mmoja.

Alihudumu kama karani katika afisi ya Wizara ya Mipangilio na Maendeleo, mnamo 1978, alipokuwa akifanya kozi fupifupi na kufanya kazi vilevile.

Baadaye, alifuzu kwa cheti cha Stashahada katika Taaluma ya Usimamizi wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Nzumbe na muda mfupi baadaye, akaajiriwa na Shirika la Kimataifa kuhusu Chakula Duniani (WFP). Akiwa WFP, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kusomea Stashahada ya Uchumi ambapo alifuzu mnamo 1994.

Alijitosa kwenye ulingo wa siasa kwa mara ya kwanza mnamo 2000 alipoteuliwa kama waziri katika Bunge la Zanzibar, na aliyekuwa Rais wakati huo, Abeid Amani Karume.Baada ya kuhudumu kwa miaka mitano, aliteuliwa tena katika wadhifa huo huo kabla ya kujinyakulia kiti cha ubunge cha Makunduchi kwa asilimia 80 ya kura, mnamo 2010.

Rais Magufuli aliponyakua ushindi, Bi Suluhu aliingia kwenye historia kama Naibu Rais wa kwanza mwanamke nchini humo na Afrika Mashariki.

You can share this post!

Magufuli aliiga Trump kupuuza corona

Utawala wa Magufuli ulikandamiza haki za kibinadamu