Rais Suluhu awahimiza Watanzania kuungana

Na SAMMY WAWERU

RAIS mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi Samia Suluhu Hassan amewahimiza raia wa nchi hiyo kuungana na kuishi kwa utangamano ili kuiboresha.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa sita wa taifa hilo, Bi Samia alisema huu si wakati wa kunyoosheana kidole cha lawama kuhusu yaliyopita.

“Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa. Tufarijiane. Si wakati wa kutazama yaliyopita, ila ni wakati wa kusonga mbele. Si wakati wa kunyoonyesheana kidole,

tuafikie yale marehemu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli alitaka,” Rais Samia akasema kupitia hotuba yake kwa taifa hilo, baada ya kula kiapo.

Bi Samia aliapishwa rasmi Ijumaa kumrithi Rais Magufuli aliyeaga dunia Jumatano.

Aidha, Bi Samia na ambaye ataongoza Tanzania kipindi ambacho Dkt Magufuli angehudumu kukamilisha awamu yake ya pili na ya mwisho, aliwarai Watanzania kushikana ili kusongesha taifa hilo mbele.

Rais Magufuli alifariki kutokana na tatizo la moyo, kwa mujibu wa maelezo ya serikali.

Hata hivyo, tetesi zinazosambazwa na wakosoaji wake, inadaiwa Dkt Magufuli aliaga dunia kutokana na virusi vya corona, alivyopinga na kupuuzilia mbali kuwepo Tanzania.

Kiongozi wa upinzani nchini humo, Bw Tundu Lissu alidai Alhamisi kwamba Rais huyo wa tano aliangamizwa na corona.

Dkt Magufuli atazikwa mnamo Machi 25, 2021 nyumbani kwake Chato, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Rais Samia amesema Tanzania itamuomboleza marehemu kwa kipindi cha muda wa siku 21, ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti.

Mazishi ya Dkt Magufuli yatakuwa ya kitaifa, ambapo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itampa heshima za mwisho kama Amiri Jeshi Mkuu.

Mizinga itafyatuliwa na kikosi cha kijeshi nchini humo. Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa kwanza Tanzania kufariki akiwa angali madarakani.

Habari zinazohusiana na hii

SULUHU APATA MPANGO TZ