• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Kizaazaa Jaji kulalama faili ya kesi ya Bobi Wine imetoweka

Kizaazaa Jaji kulalama faili ya kesi ya Bobi Wine imetoweka

NA DAILY MONITOR

KULIKUWA na purukushani katika Mahakama ya Juu Alhamisi baada ya faili ambayo jaji wa mahakama hiyo alitarajiwa kutumia kusoma uamuzi wake kuhusu ombi la kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi la kuondoa kesi la kupinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni ilipotoweka.

“Niliambia mahakama kwamba, nitasoma uamuzi wangu kuhusu maombi yote manne. Wenzangu waliamua kutohudhuria kikao leo adhuhuri,” alisema Jaji Esther Kisakye na kuongeza kuwa, alishangaa wenzake waliamua kususia kikao cha adhuhuri.

Alimlaumu Jaji Mkuu Alfonse Owiny-Dollo kwa kuagiza faili hiyo ifichwe. Alisema hangeeleza kwa kina kilichotendeka akisema ni masuala ya ndani ya mahakama ya juu zaidi katika nchi hiyo.

Jaji Kisakye alisema hayo akiketi peke yake katika mahakama baada ya muda wa mapumziko. Majaji walichukua mapumziko mafupi kabla ya kurejea kuendelea kusoma sababu za uamuzi wao kuhusu ombi ambalo Kyangulanyi aliondoa.

Hata hivyo, hawakurudi. Badala yake, mawakili wanaowakilisha Mwanasheria Mkuu, Tume ya Uchaguzi (EC), Rais Museveni na Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina Bobi Wine, walialikwa kwa mkutano mfupi ulioitishwa na Jaji Owiny-Dollo kujadili masuala kuhusu uamuzi wa Jaji Kisakye.

Mawakili waliohudhuria mkutano huo na ambao waliomba wasitajwe majina walisema kwamba, majaji walikataa kurudi kortini baada ya mapumziko kwa sababu waliahirisha kesi kuwaruhusu kusuluhisha tofauti zao na Jaji Kisakye.

Hata hivyo, Jaji Kisakye alirudi peke yake adhuhuru kusoma uamuzi wake. Aliketi kortini kwa dakika kadhaa bila faili kabla ya kurejea katika ofisi yake kuichukua.

Duru ziliambia Daily Monitor kwamba, shida ilianza baada ya Jaji Kisakye kuashiria kwamba angeandika uamuzi uliotofautiana na wenzake lakini akakataa kuwaeleza sababu za kufanya hivyo ilivyo kawaida yao majaji hao.

Inasemekana kuwa, sababu kubwa ya mzozo huo, ni uamuzi wa Jaji Kisakye wa kuandika uamuzi wake binafsi katika ombi ambalo Male Mabirizi anataka Jaji Owiny-Dollo kujiondoa kusikiliza ombi la Kyagulanyi.

Majaji wengine walikubaliana kwamba ni Jaji Owiny-Dollo ambaye angesoma uamuzi kwa sababu masuala yaliyozuka yanamhusu lakini Jaji Kisakye akaamua kwenda kinyume.

Maji hao wawili ni miongoni mwa tisa walioteuliwa kusikiliza kesi ya uchaguzi ya Bw Kyagulanyi.

Kufikia alasiri, Jaji Kisakye alikuwa akisoma uamuzi wake mbele ya wakili wa Bw Kyagulanyi, Samuel Muyizi, wanahabari na wafanyakazi wa mahakama. Mawakili wa pande nyingine katika kesi hiyo walikuwa wameondoka.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Nenda salama Magufuli

IEBC yasaka ardhi kuhamisha makao