• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
JAMVI: Raila anawazia nini iwapo atasalitiwa na Rais Kenyatta?

JAMVI: Raila anawazia nini iwapo atasalitiwa na Rais Kenyatta?

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho kupuuzilia mbali wito wa ODM kumtaka kujiondoa kutoka kwenye mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) imezua shaka miongoni mwa wandani wa kinara wa chama hicho Raila Odinga.

Dkt Kibicho ambaye amekuwa akiongoza kampeni ya kupigia debe BBI katika eneo la Mlima Kenya, Jumatano, alisema kuwa hataacha kuelimisha Wakenya kuhusu mswada huo unaolenga kurekebisha Katiba.

“Katiba ni ya kila mtu na wala si ya wanasiasa peke yao. Mimi nikiwa kama mtumishi wa serikali, nina wajibu wa kuelimisha Wakenya kuhusu mswada wa BBI. Kuna watu wanataka tunyamaze, sitanyamaza,” akasema.

Dkt Kibicho alikuwa akiwajibu wandani wa Bw Odinga; Seneta wa Siaya James Orengo na wabunge Otiende Amollo (Rarieda) na Junet Mohamed (Suna Mashariki) ambao walimtaka kuachana na BBI.

Viongozi hao wa ODM walisema kuwa watajiondoa kwenye mwafaka baina ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta endapo Dkt Kibicho ataendelea ‘kuteka nyara’ mchakato wa BBI.

Wandani wa Bw Odinga wanashuku kuwa Dkt Kibicho anaunda njama ya kutaka mmoja kati ya Seneta wa Baringo Gideon Moi, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), arithi Rais Kenyatta atakapostaafu 2022.

Bw Odinga amekuwa akitarajia kuwa ataungwa mkono na Rais Kenyatta katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao.Nduguye Raila, Oburu Odinga, amekuwa akisema kwamba uwezekano wa kiongozi wa ODM kuchaguliwa kuwa rais 2022 uko juu kwa sababu atapata uungwaji mkono kutoka kwa Rais Kenyatta.

Lakini matamshi ya viongozi wa ODM ya hivi karibuni yameashiria kwamba huenda Bw Odinga akachezewa shere na Rais Kenyatta.Kulingana na Bw Mohamed, utata uliokuwepo baina ya ODM na Dkt Kibicho tayari umetatuliwa baada ya Rais Kenyatta kuingia kati.

“Utata uliokuwepo umeisha na shughuli ya kupigia debe BBI inaendelea bila shida yoyote,” Bw Mohamed akaambia Taifa Jumapili.Lakini mdadisi wa masuala ya kisiasa Bw Mark Bichachi anasema kuwa tangu wanasiasa kutoa lalama zao hadharani wameonekana kupunguza kasi ya kupigia debe BBI.

“Bw Odinga alikuwa mgonjwa mara tu baada ya wandani wake kutoa matamshi ya kulaumu Dkt Kibicho. Viongozi wengine wa ODM pia wamesalia kimya kuhusu BBI.

“Kabla ya Rais Kenyatta kupiga marufuku mikutano ya kisiasa, tuliona Bw Moi akijaribu kuzunguka katika maeneo ya Bonde la Ufa akipigia debe BBI. Lakini viongozi wa ODM walisalia kimya. Hiyo inaweza kuwa ishara kwamba mambo si sawa,” akasema Bw Bichachi.

Wakili Felix Otieno anaonya kuwa hatua ya Kibicho kuapa kuwa ataendelea na shughuli ya kupigia debe kinyume na wito wa ODM ni ishara kwamba mvutano ungalipo.

“Ikiwa Rais Kenyatta aliingilia kati na kusuluhisha mvutano uliopo, Dkt Kibicho asingesisitiza kuwa ataendelea kupigia debe BBI. Dkt Kibicho hawezi kupuuza Rais. Hivyo, ODM wana sababu ya kuwa na wasiwasi,” anasema Bw Otieno.

Wakili Martin Oloo anasema kuwa iwapo Rais Kenyatta ataamua kumsaliti Bw Odinga, kiongozi huyo wa ODM atakuwa amelemazwa kisiasa.

“Bw Odinga atakuwa na mambo matatu ya kufanya: kuunga mkono mwaniaji atakayepewa baraka na Rais Kenyatta, kuwania kivyake kupitia tiketi ya ODM au kuungana na Naibu wa Rais William Ruto,” anasema Bw Oloo.

Anaendelea: “Bw Odinga akiamua kuungana na Dkt Ruto itabidi akubali kuwa mwaniaji mwenza. Katiba hairuhusu Dkt Ruto kuwa naibu wa rais tena baada ya kukamilisha mihula mwili. Akiunga mkono mwaniaji atakayepewa baraka na Rais Kenyatta itakuwa serikalini. Lakini wafuasi wake hawatamruhusu kuchukua nyadhifa za chini kama vile uwaziri mkuu. Ikiwania kivyake, uwezekano wa kuingia Ikulu utakuwa mfinyu.”

Baadhi ya wadadisi pia wanashuku kwamba huenda Bw Odinga akabuni muungano na wanasiasa kama vile aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Kibiashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) Mukhisa Kituyi, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kati ya wengine.Lakini Bw Javan Bigambo anasema kuwa Bw Odinga ni mwanasiasa mwenye tajiriba ambaye hafai kupuuzwa.

“Baada ya kupona, tutafuatilia kwa karibu mienendo ya kisiasa ya Bw Odinga ili tuone hatua atakayochukua. Akionyesha dalili za kukwepa BBI tutajua kwamba ameanza mikakati ya kuachana na Rais Kenyatta. Akipigia debe BBI kama ilivyokuwa hapo awali, itabidi tungojee hadi baada ya kura ya maamuzi,” anasema Bw Bigambo.

You can share this post!

JAMVI: Gumzo la ugombea-wenza Mlima Kenya lilivyo kiazi...

Wakili Karim Khan kujiondoa kwenye kesi ya Ruto ICC