• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Vigezo muhimu kuzingatia kufanikisha kilimo cha mvungulio

Vigezo muhimu kuzingatia kufanikisha kilimo cha mvungulio

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA wa vivungulio wamekumbatia mfumo huo wa kisasa kwa sababu kadha wa kadha. Ni mfumo unaosifiwa kuimarisha shughuli za kilimo, na pia kuvuna mazao bora na ya kutosha, ukilinganishwa na eneo tambarare.

Mosi, vivungulio vinapigiwa upatu kupunguza kasi ya msambao wa wadudu na magonjwa, kupitia upepo na maji. Ni changamoto ambazo hulemea wakulima wengi hasa kwa ajili ya gharama ya juu kununua dawa.

Kimsingi, kilimo cha mvungulio hudhibiti maenezi ya wadudu na magonjwa, huku wanaoingia humo wakiwa ni wanaoruhusiwa pekee na kwa kufuata mikakati na kanuni zilizowekwa.

Matumizi ya kivungulio maarufu kama greenhouse, ni mfumo wa kisasa unaotumika kuhakikisha uhaba wa chakula, haswa viungo vya mapishi haushuhudiwi.

Walioukumbatia, huzalisha mazao nyakati zozote, ikiwa wana chanzo cha maji ya kutosha, badala ya kutegemea msimu wa mvua.

Kilimo cha mvungulio kikipigiwa upatu kutokana na jitihada zake kupunguza matumizi ya dawa zenye kemikali na fatalaiza, pia kinasaidia kukabili kwekwe, na hii ina maana kuwa mazao huwa ya hadhi ya juu na salama.

Licha ya manufaa chungu nzima ya mfumo huu, si wengi walioweza kuufanikisha. Baadhi ya wakulima wamekiingilia kwa sababu ya muigo, baada ya kuona mkulima fulani anafanya bora na kuvuna hela.

Kulingana na Geoffrey Kavita, mtaalamu kutoka Amiran Kenya, tawi la Naivasha, si mimea yote inapaswa kukuziwa kwenye kivungulio. Mdau huyu wa masuala ya kilimo anasema kuna chaguo la mimea.

“Kwa waliokumbatia kilimo cha mvungulio, mimea kama vile kabichi na vitunguu haipaswi kukuziwa humo. Ni ya eneo tambarare,” Kavita anasema.

Isitoshe, kwa mimea inayoorodheshwa kulimwa humo, kuna halisi inayopaswa.

Nyanya, pilipili mboga na matango, ndiyo hukuzwa kwenye vivungulio. “Katika mimea hiyo, kuna maalum kwa mujibu wa uhalisia na changamoto zake inayopaswa kulimwa kwenye greenhouse na mingine eneo tambarare. Mfano, nyanya aina ya Anna F1, Eva F1, Tylka F1 na Nikomate F1 zinafanya bora kwenye kivungulio,” Kavita anafafanua.

Katika orodha ya pilipili mboga, anapendekeza Golden Sun F1, Indra, Admiral na Commandant, matango; Carmen, kukuziwa kwenye kivungulio.

Muhimu zaidi, ni kutambua mbegu zenye ustahimilivu wa hali ya juu kwa magonjwa na wadudu.

Kulingana na mtaalamu huyo, kinachorambisha sakafu wakulima wengi ni kukosa kuzamia utafiti wa kina kabla kufanya maamuzi kukumbatia kilimo cha mvungulio.

Anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba madhumuni ya kivungulio ni kufanikisha kilimo-biashara.

“Baada ya kutafiti mimea inayolimwa kwenye vivungulio, fahamu soko lake na namna ya kuikuza,” anashauri, akihimiza mkulima au wakulima chipukizi kutembelea walioimarika na pia kutumia intaneti kutafiti.

Anataja makosa makubwa wanayofanya wakulima kama – kukosa kuzamia utafiti wa kina kuhusu soko la mazao.

“Waliofanikinisha kilimo cha greenhouse ni wenye soko tayari, hususan waliotia saini mkataba na wanunuzi – kampuni na mashirika. Wasio na wateja, huishia mikononi mwa mawakala na ambao huwapunja kwa kununua mazao wanavyotaka,” anafafanua.

Katika mdahalo wa kuafikia kilimo bora, Kavita anasema mimea ina vigezo vitatu (mahitaji):

1. Chakula cha mimea, yaani madini faafu kwenye udongo kama vile Naitrojeni, Potasiamu, Fosforasi…kati ya mengineyo.

2. Usalama wa mimea; kukabili wadudu, magonjwa na kwekwe.

3. Mbinu ya kila mimea kuikuza.

“Kimsingi, vigezo hivyo viangazie suala la udongo kukaguliwa na kufanyiwa vipimo kwenye maabara – kujua kiwango cha asidi na alkali (pH), kukabili changamoto za wadudu, magonjwa na kwekwe. Mkulima pia aelewe mbinu faafu kutunza mimea, kama vile kupogoa matawi ili kupunguza ushindani wa lishe, ambayo ni mbolea na maji,” anasisitiza.

Huku kilimo cha mvungulio kikionekana kana kwamba ni ghali, Kavita anasema gharama yake ni nafuu na ya chini mno, ikilinganishwa na eneo tambarare.

Anahimiza wakulima kufahamu vifaa bora kutengeneza kivungulio. “Aghalabu huundwa kwa vyandarua vya karatasi ya plastiki yenye maumbile ya aina yake kuchuja miale ya jua inayopenyeza, vumbi na maji ya mvua. Kuna wanaotumia miti au vyuma, kwa mujibu wa uwezo wa mkulima kifedha,” anaelezea, akisisitiza kuhusu matunzo bora ya mimea kivungulioni.

Anaonya kwamba kero ya magonjwa inachochewa na udongo na maji yanayonyuziwa mimea na mazao.

Kwa muda mrefu, David Karira ambaye ni mkulima wa pilipili mboga na nyanya kwenye kivungulio amekuwa akihangaishwa na ugonjwa wa Bacterial Wilt na Fusarium Wilt.

“Nimetafutia magonjwa hayo dawa ila sijaipata. Yakikita kambi, majani na matawi huanza kunyauka na hatimaye kukauka. Ni hasara na pigo kwa mkulima,” analalamika mkulima huyo.

Baada ya mavuno, Karira hutandaza chandarua cheusi na kukitumia kufunika udongo kwa kipindi cha muda wa miezi sita mfululizo, ili kukabili magonjwa hayo.

Mtaalamu Kavita anasema ni magonjwa ya udongo, na ambayo husalia udongoni hata baada ya mavuno.

“Msambao wa magonjwa hayo huchangiwa na maji hususan yanayotiririka ardhini na udongo – kupitia wanaoingia kwenye kivungulio bila kudhibitiwa,” anafafanua, akihimiza wakulima kuweka maji yenye dawa kwenye kiingilio cha vivungulio ili makanyigio yenye viini visababishi yatibiwe kuviua.

Anasema magonjwa mengine husababishwa na kwekwe. Yote tisa, kumi mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji, hasa ya kusindikwa kwenye mashina ya mimea (drip irrigation) ndiyo bora kwenye kilimo cha mvungulio.

You can share this post!

Kabras sumu kwa Quins kwenye Ligi Kuu ya raga

Derby FC kupigana kufa kupona kupanda daraja