• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Serikali ilinde wote mitihani inapoanza

TAHARIRI: Serikali ilinde wote mitihani inapoanza

KITENGO CHA UHARIRI

HATIMAYE baada ya kusubiri kwa zaidi ya miezi mitano, wanafunzi wa darasa la Nane kote nchini wanapata fursa ya kuufanya mtihani wa KCPE.

Ni mtihani unaopima yale waliyojifunza katika kipindi chote cha miaka minane katika shule za msingi. Huu ni muda wa watahiniwa hao kujiamulia hatima yao, ingawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kila anayefanya mtihani huo anajiunga na shule ya upili au chuo cha mafunzo ya kiufundi.

Mtihani huu unafanywa katika mazingira tofauti kabisa na miaka ya zamani. Unajiri wakati watahiniwa hao karibu 1,191, 725 wakiwa wamepoteza miezi sita wakiwa nyumbani. Punde Kenya ilipotangaza kuwepo kwa ugonjwa wa Corona mwezi Machi, Rais Uhuru Kenyatta alifunga shule zote na vyuo wiki chache baadaye.

Wanafunzi walikaa nyumbani hadi Oktoba, serikali ilipowaruhusu wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kurudi shuleni. Lengo wakati huo lilikuwa kupata nafasi ya kutosha ya kutekeleza umbali kutoka kwa mwanafunzi mmoja hadi mwengine.

Mtihani huu unapofanywa kwa siku tatu zijazo, bado macho ya wazazi ni kuhusu usalama wa watoto wao. Kuna pendekezo kutoka kwa chama kipya cha walimu wa kike (Ketowa), kwamba walimu wakuu na walimu hasa wa shule za kibinafsi wapewe kipaumbele katika utoaji chanjo.

Huku idadi ya maambukizi ya ugonwa wa corona a vifo vikiongezeka kwa kasi, walimu wakuu, wasimamizi wa mitihani na watahiniwa ndio wanaokabiliwa na tishio kuu zaidi. Kwa siku tatu watakuwa wakitangamana kwa karibu.

Baadhi ya mapendekezo ni serikali kuwapa walimu na wasimamizi wa mitihani gari lao la kuwasafirisha, kinyume na kuwajumuisha pamoja na maafisa wa polisi katika malori ya polisi.

Pamoja na mapendekezo haya, serikali yapaswa kuweka huduma za dharura katika vituo vya mitihani. Ikiwezekana kuwe na maafisa wa afya katika vituo vya mitihani, ili kushughulikia kwa haraka masuala yoyote ya dharura.

Kawaida baadhi ya shule huwapikia watahiniwa wa darasa la Nane. Shule hufanya hivyo ili kuwazuia watahiniwa kuondoka shuleni mchana. Wapishi watakaohusika kutayarisha chakula cha wanafunzi hao pia yafaa wapimwe. Maafisa wa afya wapitie shule kuhakikisha kwamba afya ya wanafunzi na maafisa wote wanaosimamia mitihani, inalindwa dhidi ya maambukizi ya corona.

You can share this post!

Marais 10 kuhudhuria ibada ya kumuaga Magufuli Dodoma leo

WANGARI: Suluhu awe suluhu kweli kwa Tanzania na Afrika...