• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
WANGARI: Suluhu awe suluhu kweli kwa Tanzania na Afrika Mashariki

WANGARI: Suluhu awe suluhu kweli kwa Tanzania na Afrika Mashariki

Na MARY WANGARI

TAIFA la Tanzania linapojiandaa kumuaga buriani Rais John Pombe Magufuli Alhamisi, kuna mwanga wa matumaini kwamba mrithi wake Bi Samia Hassan Suluhu, ambaye anaonekana kuwa na maadili thabiti ya kijamii, ataliunganisha taifa hilo kwa njia ya kipekee.

Rais Suluhu, aliyelishwa kiapo Ijumaa wiki iliyopita, ametwikwa usukani wakati taifa hilo la bara la Afrika Mashariki, lingali linauguza athari za chaguzi kuu zilizofanyika mwishoni mwa mwaka jana, ambazo zilizingirwa na utata kiasi cha kuvutia jamii ya kimataifa.

Changamoto kuu zikiongozwa na kunyamazishwa kwa vyombo vya habari, kudhulumiwa kwa wakosoaji na wanasiasa kutoka kwa vyama vya upinzani, huku baadhi wakikimbilia hifadhi katika mataifa jirani, ni baadhi tu ya masuala yanayohitaji rais huyo kuyasuluhisha kwa dharura.

Uhalisia ni kuwa, Bi Suluhu anasubiriwa na kibarua kigumu hasa kwa kuzingatia tofauti kati yake na marehemu rais Magufuli.

Marehemu Magufuli alijishindia jina “bulldozer” kutokana na tabia yake ya utekelezaji sera kimabavu, ujasiri wa kupuuzilia mbali hadharani jumuiya ya kimataifa hasa msimamo wake kuhusu mikakati ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19, iliyomvutia sifa tele na shutuma kali kwa usawa.

Bi Suluhu kwa upande wake ni mwanamke wa Kiislamu anayefahamika kwa tabia yake ya upole na maneno machache na si ajabu kuwa wengi hawakumsikia sana Rais Magufuli alipokuwa angali hali.

Kando na hayo, Rais Suluhu aliingia katika vitabu vya kihistoria kama rais wa sita Tanzania, rais wa kwanza Tanzania ambaye ni mzaliwa wa Kisiwa cha Zanzibar, na mwanamke wa kwanza kuwa rais Tanzania na katika bara la Afrika Mashariki kwa jumla.

Bila shaka, kuna mengi yanayotarajiwa kutoka kwake sio nchini Tanzania tu bali vilevile katika bara zima kwa jumla, hali itakayomhitaji kujitahidi maradufu kuthibitisha kwamba wanawake vilevile, wanafaa na wana uwezo wa kushikilia afisi ya urais.

Ni kipindi muhimu cha kihistoria katika bara hili lililoandamwa na kasumba tele potovu kuhusu usawa wa kijinsia na ambalo bado limesalia nyuma katika juhudi za kuwajumuisha wanawake katika nyadhifa za uongozi.

Uhuru wa vyombo vya habari hata hivyo, ni suala nyeti ambalo Rais Suluhu ni sharti alipatie kipaumbele, hasa baada ya taharuki, sintofahamu na utata uliozingira hali ya kiafya ya Magufuli, kuugua na hata kufariki kwake.

Baada ya uhuru wa wanahabari kuhusu kufahamisha umma kuvurugwa Tanzania, katika juhudi za kutafuta ukweli, umma ulikimbilia mitandaoni ambapo matokeo yake yalikuwa kuenezwa kwa uvumi na propaganda za kila aina.

Tanzania na Afrika Mashariki inapofungua ukurasa mpya chini ya uongozi wa rais mwanamke, ni matumaini kwamba Rais Suluhu, sawia na maana ya jina lake, atakuwa suluhisho linalohitajika Tanzania na Afrika kwa jumla.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ilinde wote mitihani inapoanza

ONYANGO: Magufuli alikuwa mtetezi sugu wa wanyonge halisi