Pasta afokewa kupendelea vipusa

Na TOBBIE WEKESA

BUCHINGA, Mumias

KIOJA kilizuka katika kanisa moja la eneo hili baada ya mapolo kumzomea pasta wakidai kwamba alikuwa akipendelea vipusa katika mahubiri yake.

Kulingana na mdokezi, mara kwa mara, pasta alikuwa akiwapendelea sana wanawake wakati akitoa mafunzo yake kanisani jambo ambalo halikuwafurahisha mapolo.

Duru zinasema ili kudhihirisha gadhabu yao, makalameni waliamua kumkabili mtu wa Mungu. Siku ya kioja, pasta alijongea kwenye altari na kuanza kuhubiri ilivyokuwa desturi yake. Inadaiwa baada ya kunukuu kifungu cha Bibilia, pasta alianza moja kwa moja kuwadhalalisha mapolo.

“Wasichana ninataka kuzungumza nanyi. Mungu anawapenda sana. Endeleeni kumheshimu Mungu naye atawatimizia matamanio ya mioyo yenu,”pasta alihubiri.

Baadaye pasta aliwageukia mapolo. “Ninataka wanaume wote ambao hawajapata jiko wanisikilize kwa makini. Kila siku mnakuja hapa kunitazama tu. Mungu amekataa kuwabariki kwa sababu hamjui kuomba,” pasta aliwafokea.

Inadaiwa makalameni waliangaliana kisha wakasimama wote kwa pamoja. “Kama hatujui kuomba mbona hutaki kutufunza,” sauti ya polo mmoja ilisikika ikisema.

Vicheko vilisikika kote kanisani. “Mwaka huu ni mwaka wa urejesho kwa akina dada,” pasta aliendelea kusema.

Habari zilizotufikia zinasema mapolo walipandwa na za kwao na kuanza kumfokea pasta. “Kwenda huko. Umetudharau sana kwa muda mrefu. Tumechoka na hizo kejeli zako,” walifoka. Pasta alianza kutokwa na kijasho jembamba.

“Mahubiri yako yamejaa mapendeleo na madharau mengi sana. Unawapendelea warembo sana sijui wana nini ambacho sisi hatuwezi kukupa,” polo mmoja alimzomea pasta.

Pasta alitamani ardhi ipasuke immeze mzimamzima. “Koma hiyo tabia ama tuhame kanisa,” makalameni walionya na kuketi chini huku pasta akibadilisha mahubiri.

Yasemekana baada ya ibada aliwaita makalameni kwa mkutano na kuwaomba msamaha akisema hakuwa na nia mbaya kwao.