Usalama waimarishwa katika mpaka wa Kenya na Somalia watahiniwa wakifanya KCPE

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI imeimarisha usalama kwenye mpaka wa Kenya na Somalia wakati huu ambapo mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) unaendelea.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amesema maafisa wa usalama wamesambazwa kwenye shule za maeneo hayo ili kuona kwamba mtihani wa KCPE unafanywa bila kutatizwa.

Baadhi ya shule zilizoko kwenye eneo la mpaka wa Kenya na Somalia ni pamoja na Kiunga, Ishakani, Mkokoni na Kiwayu.

Jumatatu, Bw Macharia, akiandamana na maafisa wengine wakuu wa idara ya usalama eneo hilo wamezuru Shule ya Msingi ya Kiunga, ambapo wamekagua madarasa ambayo yanatumiwa na watahiniwa na vile vile kuongoza shughuli ya kufungua kontena za karatasi za mtihani mjini Kiunga.

Kamishna huyo amewataka wanafunzi, wazazi, walimu na wasimamizi wa mtihani kuondoa shaka na kuwahakikishia kuwa usalama wao umedhibitiwa vilivyo.

Bw Macharia pia amewaonya wenye nia ya kutekeleza udanganyifu kwenye mtihani huo kwamba serikali iko macho na itawaandama.

“Lengo letu hasa ni kukagua hali ya madarasa na pia kutathmini usalama eneo hili wakati KCPE ikiendelea,” akasema Bw Macharia.

Katika kisiwa cha Lamu, Mkurugenzi Mkuu wa Elimu, Joshua Kaaga ameongoza maafisa wengine wa elimu katika shughuli ya kufungua kontena ya karatasi za mtihani iliyoko mkabala na ofisi ya Naibu Kamishna wa Lamu.

Kulingana na Bw Kaaga, jumla ya wanafunzi 3,348 wanafanya KCPE kote Lamu mwaka huu 2021.

Idadi hiyo ni ya chini ikilinganishwa na mwaka 2019, ambapo wanafunzi wote waliofanya mtihani huo walikuwa 3,673.

Takwimu za mwaka huu zinaonyesha kuwa wanafunzi wa kike wanaofanya KCPE Kaunti ya Lamu ni wengi ikilinganishwa na wenzao wa jinsi ya kiume.

Kati ya wanafunzi 3,348, wale wa kike ni 1,705 ilhali wa kiume ni 1,643.

Mwaka huu Lamu iko na jumla ya vituo vya mtihani wa KCPE 92 ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo vituo hivyo vilikuwa 95.

“Matarajio yetu ni kwamba watahiniwa wote watafanya mtihani huo kuanzia sasa, ikizingatiwa kuwa wote walifika shuleni Ijumaa wakati wa shughuli ya maandalizi. Nawatakia kila la heri nikiwasihi wajiepushe na udanganyifu,” akasema Bw Kaaga.

Katika eneo la msitu wa Boni, wanafunzi wote wa Darasa la Nane kutoka jamii ya Waboni wanafanya mtihani huo kwenye Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone.

Shule za msitu wa Boni zikiwemo Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe na Bodhai zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya mara kwa mara ya mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa al-Shabaab, ambapo shule hizo zililazimika kufungwa kwa zaidi ya miaka saba.

Mwaka huu, serikali ilizifungua shule hizo lakini ikaamuru wanafunzi wa chekechea hadi Gredi ya Nne pekee wafundishwe kwenye shule hizo za msitu wa Boni ilhali wale wa madarasa ya juu wakiendeleza masomo yao kwenye shule hiyo ya msingi ya bweni ya Mokowe Arid Zone.

Habari zinazohusiana na hii