• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ndani ya ndoto ya wahudumu wa bodaboda wa Kangema ya kuwa mabilionea kuelekea mwaka 2027

Ndani ya ndoto ya wahudumu wa bodaboda wa Kangema ya kuwa mabilionea kuelekea mwaka 2027

Na MWANGI MUIRURI

KATIKA miaka ya sitini – 1960s – vijana barobaro lakini waliokuwa na mizizi ya umasikini kutoka kijiji cha Rwathia eneo la Kangema walizindua harakati za kujiwekea akiba na kuwekeza katika sekta ya vipande vya ardhi na nyumba.

Vijana hao licha ya kuwa na elimu duni walijinyima anasa za kimaisha na wakakubali kurarukiwa na kula lishe duni wakijua tu ni kwa ,muda, na wakaweza kujipa mashiko ya kifedha kupitia akiba ya pesa za mauzo ya majanichai, kahawa na pia uchomaji makaa na uuzaji wa mbao za ujenzi.

Katika uzee wao, walikuwa wamefanikiwa kumiliki majumba makubwa na vipande vya ardhi katika miji kadha ya hapa nchini, likiwemo Jiji la Nairobi, Thika, Nakuru na Murang’a na la mno, wakaelimisha watoto wao.

Hao ndio wazee ambao walishawishi watoto hao wavulana kupenda elimu na kutia bidii katika ajira zao kiasi kwamba Rwathia kuliishia kuwa ngome ya mabilionea ambao leo hii ndio wanatesa katika safu ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa chapisho la 2014 la aliyekuwa Katibu Maalum katika Wizara ya Habari na Teknolojia Dkt Bitange Ndemo kwa utambuzi: The Mystery of Success (Maajabu ya Ufanisi), anasema kuwa Wadi ya Rwathia huwa na mabwanyenye katika uchumi wa taifa hili ambao hudhibiti takriban asilimia 20 ya pato lote la taifa (GDP).

Anasema kuwa mabwanyenye hao hudhibiti zaidi ya nusu ya soko la hisa hapa nchini huku kizazi cha tatu cha familia za mabyanyenye hao kikiwa kinanawiri vyema katika safu za elimu na biashara hapa nchini na hata Ulaya kwa kuwa waliwekewa jiwe la msingi lililo thabiti; nao wakatii na wakafuata nyayo za akina babu wakiwa na nidhamu ya kifedha.

Ushawishi huo ndio umewatuma wahudumu wa bodaboda katika kaunti ndogo hiyo ya Kangema kuzindua mikakati ya kujiimarisha na katika ndoto zao, wanalenga kuwa wamejiweka katika mkondo wa ukwasi wa kiwango cha ubilionea kabla ya mwaka wa 2026 kuisha.

Wanasema ile barabara ya akiba na uwekezaji ambayo baadhi ya mababu wa Kangema walifuata katika miaka ya 60’s na wakafanikiwa, huku mababu wengine wakiwaona kama wajinga na badala ya kujiunga na utekelezaji wa njama ya kuimarisha maisha yao ya kifedha waliamua kuingia kwa mtindi na wakaacha urithi tu wa umasikini, ndiyo njia watafuata ndio historia ikiendelea kuandikwa kuhusu Rwathia, isifioke wakati itaandikwa kuhusu jinsi mabilionea waliisha Kangema.

Katika ndoto hii yao, wamejigawa katika vikundi vitatu kutoka wadi za Rwathia, Muguru na Kanyenyaini ambapo idadi yao wanasema ni 3, 500.

Madiwani Peter Mweri, Jeremiah Kihara na Maina Ngundo wa wadi hizo mtawalia wanasema kuwa wamefurahishwa sana na ufumbuzi wa ndoto hiyo miongoni mwa wanabodaboda wa eneo hilo na wanaomba serikali ya Kaunti ya Murang’a sambamba na ile kuu zimakinikie ubunifu huo na zitoe jeki yao ya kifedha kwao.

“Kwa kweli hii ni habari njema kutoka kwa vijana wetu wa bodaboda ambao wanataka kuitoroka ile nembo ya jadi ya wahudumu katika sekta hii ambao huhusishwa tu na umang’aa, utumizi wa mihadarati na pombe haramu, kujiingiza katika kila aina ya ukora wa uchukuzi na mapenzi kiholela kwa mabibi za wenyewe na watoto wa shule,” asema Bw James Kariuki, mshirikishi wa vuguvugu la “Vijana Tugutuke” eneo la Kengema.

“Kinyume na mababu hao wetu ambao walizindua ndoto yao ya kusaka ukwasi wakiwa hawana elimu na kukiwa na sekta ya teknolojia ambayo ilikuwa analogu, wakiwa hawana wa kuwasaidia kukusanya mtaji; sisi hatuna la kutukwamiza bali tunachohitajika kufanya ni kamua na kujituma kuweka akiba na kuwekeza na turatibu,” asema Bw James Gituku, mwanachama wa kamati ambayo inaunda utekelezaji wa ndoto hii ya wanabodaboda hao.

Bw Gituku anasema kuwa “sisi tumeelimika hata ikiwa wengi ni kwa viwango vya sekondari, tuko na ufahamu wa ulimwengu wa Kiteknolojia na tuko na mashiko katika afisi za uongozi ambapo tunaweza tukajitetea tusaidiwe na mtaji. Pia sekta za kifedha na uongozi zimestawi kiasi kwamba kuna hazina tele ambazo tunaweza tukalenga na hatutauza makaa ndio tufanikiwe.”

Anasema kuwa ndoto hii yao itatekelezwa kupitia kuunda vyama vya ushirika vya bodaboda wa Rwathia, Muguru na Kanyenyaini kisha mashirika hayo madogo yawe yakiratibiwa na muungano mkuu wa ushirika wa wanabodaboda wa Kangema.

Katika uratibu wa muungano huo wa ushirika, wanabodaboda hao wanasema wataunda Kamati kuu ya kuongoza uwekezaji na ambapo waliokubali kuwa katika kamati hiyo ni mabwanyenye tajika kama Dkt James Mwangi ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya Equity, Bw Peter Kahara Munga ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa Benki hiyo na wawekezaji Benson Wairegi na Jimnah Mbaru ambao wote ni miongoni mwa Mabilionea wa Kangema.

Kwa mujibu wa Bw Johnson Mukuha ambaye ndiye mshirikishi wa mpango huu ambao umepewa utambuzi wa Kangema Bodaboda Youths Vision 2026 “tunataka kufuata nyayo za walioweka msingi wa eneo hili la Kangema kuwa na sifa za sasa za kuwa ngome ya mabilionea.”

Bw Mukuha ambaye ni wa familia moja na Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta, anasema: “Kile tu tunalenga ni kuharakisha ratiba ya kufanikiwa kwa kuwa idadi yetu ni kubwa na katika uratibu wa makundi ya ushirika, ni busara kuwekeza kwa haraka ndiposa pesa zinazotolewa kama akiba zianze kuleta faida ya haraka na kwa wingi kwa kasi inayofaa.”

“Ratiba yetu ndiyo hii: Tukiwa na wanachama 3,500 katika ushirika wetu na kila mmoja awe akiweka akiba ya Sh50 kwa siku, pesa ambazo zitatokana na ujumlishaji wa kila mwezi ni Sh5.25 milioni. Kwa mwaka hizo ni Sh63 milioni,” afichua.

Hisibati za Bw Mukuha katika safari ya kutimiza ndoto hii ni kuwa, katika ukadiriaji wa idara za mikopo ambapo akiba huvutia mkopo unaolingana na mara nne ya akiba, kwa mwaka wa kwanza watakuwa na uwezo wa kujipa mkopo wa Sh252 milioni.

“Ikiwa tutaweka akiba hii yetu kwa miaka mitano mfululizo, akiba yetu itakuwa imetinga Sh615 milioni na ambapo uwezo wetu wa mikopo utaruka hadi Sh1.26 bilioni na ambapo tutakuwa na uwezo wa kuzindua hata benki yetu kabla ya mwaka wa 2026 kuisha,” asema.

Anasema kuwa kwa sasa kila mwanachama anatakikana kujisajili na Sh1, 000 ambapo pia ukwasi wao wa pamoja utakuwa Sh350,000 na ambao utakuwa akiba anzilishi katika akaunti yao.

Tayari Naibu Rais Dkt William Ruto amewatembelea vijana hao na ambapo aliwapiga jeki ya Sh2.8 milioni.

“Hilo linakudhihirishia kuwa hatuna mchezo na kwamba kuna uwezekano wa kuanza maisha yako kutoka kwa baiskeli, upande pikipiki, upande hadhi na uendeshe gari na hata uishie kujipa ndege yako ya usafiri binafsi. Hizi sio hekaya za Abunwasi bali ni kichocheo kizuri cha kujiamini na kujipa sababu ya kuweka akiba kwa nidhamu kuu,” asema Bw Mukuha.

You can share this post!

Chiefs yakaribisha Mkenya Teddy Akumu ikirarua Orlando...

Benevento yadidimiza matumaini ya Juventus kutwaa taji la...