• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Uhuru awahimiza Watanzania kuunga mkono Rais wao Samia Suluhu Hassan

Uhuru awahimiza Watanzania kuunga mkono Rais wao Samia Suluhu Hassan

Na SAMMY WAWERU

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imepoteza mchapakazi aliyetaka kuiona ikiboreka kiuchumi, amesema Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake katika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma, Jumatatu katika hafla ya kumuaga Dkt John Pombe Magufuli – Rais wa awamu ya tano Tanzania – aliyefariki Machi 17, 2021.

Rais Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa EAC amemtaja Dkt Magufuli kama kiongozi aliyeheshimu Kanda ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

“Tumempoteza kiongozi mchapakazi na Rais aliyeheshimu Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla,” akasema Rais Kenyatta akitoa salamu za pole za Kenya na pia kwa niaba ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mahsariki.

Akiorodhesha miradi ya maendeleo aliyotekeleza nchini Tanzania, Rais Kenyatta alisema Dkt Magufuli ameonyesha kwamba Waafrika wanaweza kujikomboa na kujisimamia bila kutegemea mataifa ya Ulaya.

“Chini ya muda mfupi, tumeona Dkt Magufuli amefanikisha miradi ya maendeleo kama vile kuweka stima na kuimarisha barabara ambazo zitaifaa Afrika Mashariki,” akasema Rais Kenyatta.

Akaeleza: “Ninamuomboleza rafiki wa karibu, ambaye tulizungumza mara kwa mara, mchana, jioni tukijadiliana namna na jinsi ya kuboresha uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Akiahidi Kenya kuendelea kushirikiana na Tanzania, Rais Kenyatta amewataka raia wa nchi hiyo kuunga mkono Rais mpya, Bi Samia Suluhu Hassan aliyeapishwa rasmi juma lililopita kumrithi mwendazake.

Bi Samia alikuwa makamu wa Rais Magufuli.

“Dadangu Samia Suluhu, Rais mwenzangu, barabara ulionyeshwa na Dkt John Pombe Magufuli na imefunguliwa. Wito unao, tufanye kazi. Raia wa Tanzania ninawaomba mumuunge mkono aendeleze kazi iliyoanzishwa na marehemu,” akahimiza Rais Kenyatta.

Dkt Magufuli alichaguliwa kuwa Rais mwaka wa 2015, na katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita, 2020 akahifadhi kiti chake.

Serikali ya nchi hiyo ilisema alifariki Machi 17, 2021, baada ya kuugua.

Aidha, Mama Samia Suluhu alisema alifariki kutokana na tatizo la moyo, kauli ambayo pia imetiliwa mkazo Jumatatu.

Ameacha mjane, Bi Janeth Magufuli, watoto saba na wajukuu kadha.

You can share this post!

Madaktari 24 wafuzu MKU

Hit Squad yasubiri droo kabla ya mapigano ya mataifa 11...